Makala

Zawadi kwa vijana wenye vumbuzi kuboresha kilimo

March 20th, 2024 2 min read

NA SAMMY WAWERU

HEIFER International ni mojawapo ya kampuni na mashirika yanayotambua mchango wa vijana Kenya kuboresha shughuli za kilimo. 

Utambuzi huo, ni zawadi wanazotoa kwa vijana wenye bunifu katika sekta ya kilimo, Adesuwa Ifedi, Naibu Rais wa shirika hilo lisilo la kiserikali (NGO), akisema unawapa motisha kuikuza.

Tuzo hiyo, maarufu kama AYuTe Competition, Bi Ifedi anasema inahamasisha vijana kuwa na ari kushiriki kilimo.

Aidha, inalenga vijana wenye bunifu na teknolojia kufanikisha sekta ya kilimo.

“Vijana wamebobea katika masuala ya teknolojia, na ni muhimu kutambua vumbuzi zao katika kilimo,” afisa huyo mkuu anasema.

Kauli yake inatiliwa mkazo na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu tawi la Heifer Kenya, Esta Kamau akielezea haja ya kutambua mchango wa vijana.

Wakiwekwa kwenye mtandao wa uzalishaji chakula, watasaidia kwa kiwango kikubwa kuongeza mazao.

John Waweru, mmoja wa vijana waliotuzwa kupitia AYuTe Competition 2022, mpango wa Heifer International kutambua jitihada za vijana kukuza sekta ya kilimo. PICHA|SAMMY WAWERU

Hatua hiyo, aidha, italetea nchi na Bara la Afrika afueni katika jitihada kuangazia pengo la uhaba na usalama wa chakula.

“Kilimo kitaimarika vijana wakijumuishwa kikamilifu katika sekta, hasa kwa kutambua wenye bunifu na teknolojia za kisasa kunawirisha mazao, kuyaongeza thamani na pia kuunganisha wakulima kwa wanunuzi – soko,” Esta anasema.

Kilimo ni sekta pana na inayochangia zaidi ya asilimia 70 ya nguvukazi Kenya, na Esta anasisitiza haja kutambua jitihada za wanaoshiriki kwenye mitandao tofauti ya zaraa.

Inaanzia uzalishaji, utunzaji mazao na mavuno kupitia teknolojia na bunifu za kileo, bila kusahau ukumbatiaji mifumo ya kidijitali kuboresha mazao na kuyatafutia soko.

Kupitia AYuTe Challenge, mwaka huu, 2024, Heifer itatuza vijana watakaoibuka washindi kwenye teknolojia, mifumo na bunifu kuendeleza kilimo, Makala ya Nne.

John Waweru akipewa ‘kombe’ la shime baada ya kuibuka kidedea katika kinyang’anyiro cha AYuTe Competition 2022. PICHA|SAMMY WAWERU

Septemba 2023, Heifer International ilizindua Shindano la Makala hayo ambapo wabunifu wanatakiwa kuingia kwenye tovuti yake na kueleza sera zao kuboresha kilimo.

Aidha, washindi hupewa pesa na mafunzo jinsi ya kuendeleza kilimo kitaalamu na kuunganishwa kwa mianya ya soko.

Vijana wenye programu mbalimbali na bunifu kuboresha sekta ya kilimo wanahimizwa kutuma maombi.

John Waweru, mwasisi wa Optimerce Consulting Ltd, kampuni inayosaidia wakulima kupata huduma kwa njia ya kidijitali, 2022 alituzwa na Heifer International kutokana na mchango wake kwenye kilimo.

Grace Kyarimpa, kijana mwingine aliyetambuliwa na kutuzwa kupitia AYuTe Competition 2022, mpango wa Heifer International kutambua jitihada za vijana kukuza sekta ya kilimo. PICHA|SAMMY WAWERU

Shirika hilo linaamini vijana wanavutiwa na teknolojia za kisasa, hivyo basi kwa kuwateka kupitia utambuzi itakuwa rahisi kuangazia ajenda ya usalama wa chakula nchini na hata kusaidia kubuni nafasi za ajira.

Kando na tuzo hiyo, Heifer International kwa ushirikiano na Hello Tractor, inaendeleza mpango kupiga jeki wakulima kumiliki trekta.

Aidha, wenye nia wanapewa fursa ya kulipa polepole mkataba ukiwa malipo kufanywa trekta inapopata biashara – kulimia watu mashamba.

Hello Tractor huweka kila trekta mtambo kufuatilia utendakazi.

Vijana waliotuzwa kupitia AYuTe Competition 2022, mpango wa Heifer International kutambua jitihada zao kukuza sekta ya kilimo. PICHA|SAMMY WAWERU