Michezo

Zawadi ya bathdei ya Ronaldo ni gari la Sh14.9 milioni

February 6th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MWANASOKA tajiri duniani Cristiano Ronaldo alikuwa na siku yake ya kuzaliwa ya kukata na shoka mnamo Februari 5. Mpenzi wake Georgina Rodriguez alimpatia gari la kifahari kama zawadi ya kusherehekea kufikisha umri wa miaka 35.

Mshambuliaji huyo wa Juventus, ambaye utajiri wake ni Sh45.2 bilioni, sasa ana kundi la magari 20 ya kifahari. Georgina alimnunulia gari jipya la aina ya Mercedes AMG G63.

Baada ya chakula cha jioni katika hoteli ya Ristorante Casa Fiore mjini Turin, Ronaldo, ambaye hakuwa na habari kabisa kuhusu zawadi hiyo, alionyeshwa gari hilo ambalo bei yake inaweza kufika Sh14.9 milioni. Lilikuwa limepambwa na kufungwa kwa kutumia riboni nyekundu.

Georgina, ambaye alizaliwa Januari 27 mwaka 1995 (ripoti zingine zinasema alizaliwa 1990), aliunda video fupi ya Mreno huyo kwenye mtandao wa Instagram. Video ilionyesha mwanasoka huyo akisalimia marafiki na mashabiki akiwemo kifunguamimba Cristiano, Jr, ambaye ana umri wa miaka tisa.

Akitoa maelezo ya video hiyo katika lugha yake ya mama ya Kihispania, alisema, “Hongera kidume changu! Matamanio yangu ni kusafirisha mapenzi yetu katika zawadi hii yako.”

Gari hilo linaaminika kuwa mojawapo ya magari yenye uwezo wa kuendeshwa kwenye barabara laini ama ilio na mawe. Linaweza kutumia sekunde nne pekee kutoka lianzishwe likiwa limesimama na kufikia mwendokasi wa karibu kilomita 100 kwa saa.

Baada ya miaka tisa akichezea Real Madrid, Ronaldo alisaini kandarasi ya miaka minne na Juventus mwaka 2018. Jezi 520, 000 za Ronaldo ziliuzwa chini ya saa 24 alipotua Juventus zikiletea klabu hiyo zaidi ya Sh6.0 bilioni.

Ronaldo ana watoto wanne – Alana Martina dos Santos Aveiro, Eva Maria Dos Santos, Cristiano Ronaldo Jr., na Mateo Ronaldo.

Baadhi ya aina ya magari Ronaldo anamiliki ni Mercedes C Class Sport Coupe, Rolls-Royce Phantom, Ujn Ferrari 599 GTO, Lamborghini Aventador LP700-4, Aston Martin DB9, McLaren MP4 12C na Bentley Continental GTC Speed.