Zeddie Lukoye awasilisha barua Waislamu wamsamehe kwa kutumia nembo ya msikiti vibaya

Zeddie Lukoye awasilisha barua Waislamu wamsamehe kwa kutumia nembo ya msikiti vibaya

Na KALUME KAZUNGU

MWANAMITINDO wa mavazi, Zeddie Lukoye, Jumatano alisalimu amri na kujitokeza kuomba msamaha kufuatia tukio ambapo alirembesha nguo kwa kutumia picha ya msikiti wa Riyadha ulioko kisiwani Lamu.

Tishati hizo baadaye ziliishia kutumiwa katika mazingira ambayo yanakiuka maadili ya dini, hivyo kusababisha viongozi wa kidini, wazee wa Kiislamu na wasimamizi wa msikiti huo mkongwe kumshurutisha Bw Lukoye kuwaomba radhi.

Shinikizo hizo pia zilichangiwa na kisa ambapo picha ya mwanamuziki mashuhuri wa Amerika, Shawn Carter, almaarufu Jay-Z ilisambazwa mitandaoni akiwa amevaa tishati iliyo na nembo ya msikiti wa Riyadha.

Katika barua yake aliyotuma kwa wasimamizi wa msikiti wa Riyadha, Bw Lukoye alikiri kwamba alifanya makosa kuchapisha tishati zake kwa kutumia nembo ya msikiti huo bila idhini.

Alisema anajutia kwani hakuwa na ufahamu wa iwapo harakati zake za kujaribu kuiuza Lamu, hasa utamaduni na historia yake kwa kutumia nembo hiyo ya msikiti zingeibua ghadhabu.

Aliuhakikishia usimamizi wa msitiki Riyadha kwamba licha ya kuchapisha tishati 20 pekee, zile chache walizoziuza watahakikisha wanawafuata wateja wao ili kuwashauri wasizivae na kuingia nazo kilabu au sehemu nyinginezo kunakokiukwa mafunzo na misingi ya dini.

Bw Lukoye pia aliahidi kuondoa nembo aliyochapisha kwenye tishati zilizobakia na kwamba anatoa pole kwa usimamizi wa msikiti huo pamoja na mwanzishili wake, Habib Swaleh.

“Tunaheshimu dini, mila na desturi za mahali kama Lamu na ndiyo sababu tukajitokeza kuomba radhi kwa yaliyotokea kuhusu picha ya msikiti,” akasema Bw Lukoye.

Katibu wa Msikiti wa Riyadha, Abubakar Badawy alithibitisha kupokea waraka huo kutoka kwa mwanamitindo Zeddie Lukoye.

Katibu wa Msikiti wa Riyadha, Abubakar Badawy. Picha/ Kalume Kazungu

Alisema wamekubali kumsamehe mwanamitindo huyo na kuahidi kwamba watashirikiana naye ili kuinua hadhi ya Lamu kwa uzuri zaidi.

“Usimamizi wa kituo cha elimu na Msikiti wa Riyadha umepokea ombi kutoka kwa Zeddie Lukoye akitaka asamehewe na tumelikubali na hata tuko tayari kushirikiana nao katika kuikuza Lamu yetu,” akasema Bw Badawy.

Mwenyekiti wa Muungano wa Viongozi wa Dini ya Kiislamu, Mohamed Abdulkadir pia alipongeza hatua ya mwanamitindo huyo kujitokeza haraka na kuomba msamaha.

 

Mwenyekiti wa Muungano wa Viongozi wa Dini ya Kiislamu, Mohamed Abdulkadir. Picha/ Kalume Kazungu

Aliwataka wanamitindo wengine kuiga mfano wa Bw Lukoye na kuomba msamaha wanapokosea.

“Tunashukuru kwamba kilio chetu kilisikika, hivyo mwanamitindo kujitokeza na kuomba msamaha. Hili liwe funzo kwa wanamitindo wote wanaokuja Lamu. Lazima watafute ushauri kwanza kabla ya kufanya maamuzi yoyote, iwe ni ya kijamii au kibiashara,” akasema Bw Abdulkadir.

Msikiti wa Riyadha ndiyo mkongwe zaidi Lamu. Ulianzishwa mwaka 1892.

  • Tags

You can share this post!

Muungano wa makanisa chini ya mwavuli wa FEICCK walaani...

Kang’ata amtaka Matiang’i arekebishe notisi...