Michezo

Zenit St Petersburg yamsajili beki matata Dejan Lovren

July 28th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Zenit St Petersburg kimemsajili beki matata wa Liverpool, Dejan Lovren kwa mkataba wa miaka mitatu ambao umegharimu kima cha Sh1.5 bilioni.

Nyota huyo mzawa wa Croatia, 31, anaingia katika sajili rasmi ya miamba hao wa soka ya Urusi baada ya kusakata jumla ya mechi 10 za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) akivalia jezi za mabingwa Liverpool msimu huu.

Lovren alisajiliwa na Liverpool kutoka Southampton kwa kima cha Sh2.8 bilioni mnamo Julai 2014 na akawa sehemu ya kikosi kilichosaidia Liverpool kunyanyua ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2019.

Katika jumla ya mechi 131 alizowawajibikia Liverpool, alipachikwa wavuni mabao matatu matatu japo alichezeshwa mara tatu pekee katika mwaka wa 2020.

Lovren aliisaidia pia timu ya taifa ya Croatia kutinga fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2018 ila wakazidiwa maarifa na Ufaransa waliowatandika 4-2 na kunyanyua ubingwa. Amevalia jezi za Croatia mara 57 hadi kufikia sasa.

Mkataba wake kambini mwa Liverpool ulitarajiwa kutamatika rasmi mnamo Juni 2021 huku miamba hao wa soka ya Uingereza wakiwa na fursa ya kurefusha zaidi kipindi cha kuhudumu kwake ugani Anfield kwa mwaka mmoja zaidi.

“Nguli mwingine wa soka kambini mwa Liverpool ameondoka ugani Anfield. Amekuwa sehemu muhimu katika kampeni za kikosi hiki tangu siku ya kwanza nilipoajiriwa na Liverpool,” akasema kocha Jurgen Klopp aliyeaminiwa fursa ya kudhibiti mikoba ya Liverpool mnamo Oktoba 2015.