Zesco yazoa ushindi wa10 mfululizo ligini Zambia, Were, Makwata na Otieno walianza mechi

Zesco yazoa ushindi wa10 mfululizo ligini Zambia, Were, Makwata na Otieno walianza mechi

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Jesse Were, John Makwata na Ian Otieno wote walianza katika kikosi cha Zesco United ikizoa ushindi wake wa 10 mfululizo kwa kuchabanga Nkwazi 2-1 kwenye Ligi Kuu ya Zambia, Jumamosi.

Zesco, ambayo ilipigwa na Nkwazi 1-0 nyumbani na ugenini msimu uliopita, ililipiza kisasi kupitia mabao ya Kelvin Kampamba na mchezaji wa akiba Luwawa Kasoma.

Kipa Otieno alipangua kombora la Andrew Mupande dakika ya nane naye mshambuliaji Makwata akakosa nafasi nzuri dakika ya 12 kabla ya Kampamba kupachika bao safi dakika ya 26.

Makwata alipoteza nafasi nzuri dakika ya 29 na tena 38 huku kipindi cha kwanza kikikatika bila mabao zaidi. Mvamizi Were alipumzishwa dakika ya 60 na nafasi yake kujazwa na Luwawa wakati kocha Numba Mumamba alifanya mabadiliko matatu mara moja.

Makwata alikosa nafasi nyingine murwa dakika ya 66. Luwawa aliimarisha uongozi wa Zesco dakika ya 80.

Nkwazi, ambayo ilikuwa nyumbani, ilipata bao la kujiliwaza kutoka kwa Christopher Zulu dakika chache baada ya Makwata kupumzishwa.

Zesco inaongoza ligi hiyo ya klabu 18 kwa alama 55 baada ya kujibwaga uwanjani mara 25. Zanaco ni nambari mbili kwa alama 46 kutokana na michuano 26.

NAPSA Stars ambayo imeajiri Wakenya beki David ‘Calabar’ Owino Odhiambo na kipa Shaaban Odhoji na Nkana anayochezea kiungo mshambuliaji Duke Abuya ziko katika mduara hatari wa kutemwa.

Stars inakamata nafasi ya 15 kwa alama 30. Imesakata mechi 23. Itazuru Prison Leopards hapo Jumapili. Nkana ni ya 17 kwa alama 22 kutokana na michuano 24. Itakuwa ugenini dhidi ya Power Dynamos hapo Mei 9. Nkwazi ni ya nane kwa alama 38.

  • Tags

You can share this post!

CHOCHEO: Asali sio leseni ya ndoa

Waandishi wanaofanyia kazi zao Kiambu wapewa hamasisho