Zetech ndio mabingwa wapya wa karate katika mashindano yaliyoandaliwa JKUAT

Zetech ndio mabingwa wapya wa karate katika mashindano yaliyoandaliwa JKUAT

Na LAWRENCE ONGARO

MASHINDANO ya karate ya JKUAT Open Day Martial Arts, yalivutia klabu 10 zilizoshiriki.

Klabu ya chuo cha Zetech kilichoko Ruiru, iliibuka mshindi kwa kuzoa medali nne za dhahabu, fedha moja, na shaba moja.

Wenyeji – Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) cha Juja – walikamata nafasi ya pili kwa kuzoa dhahabu tatu, fedha mbili, na shaba tatu.

Nayo Thika Budokan Karate Club, ilitulia kwenye nafasi ya tatu ikitosheka na dhahabu mbili, fedha mbili, na shaba tano.

Kocha wa Thika Budokan Karate Club, Nelson Ndung’u aliridhika na matokeo hayo akisema kikosi chake kilijitahidi kuzoa medali tisa.

“Vijana wangu walifanya mazoezi kabambe kwa zaidi ya mwezi mmoja. Ni matumaini yangu kwamba katika mashindano yajayo, watafanya vyema,” akasema kocha Ndung’u.

Mkurugenzi wa michezo JKUAT, Waweru Kamaku, alizipongeza klabu zote zilizohudhuria mashindano hayo akisema wachezaji walionyesha nidhamu ya hali ya juu.

“Ninawapongeza wakufunzi wote waliohakikisha klabu zao zinacheza katika mashindano haya. Wanamichezo nao wameonyesha ujuzi wao wa kurusha mateke,” akasema mkurugenzi huyo.

Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) kilikamata nafasi ya nne kwa kupata dhahabu moja, na fedha mbili. Hakikupata nishani ya shaba.

Klabu ya Dilpack Karate ya Nairobi, ilipata dhahabu moja, fedha moja na shaba mbili.

Nayo Eagle Karate Club ya Embakasi ilijishindia dhahabu moja pekee. Hawakupata fedha na shaba.

Maji House ya Nairobi ilizoa fedha mbili bila dhahabu na shaba.

Chuo cha Machakos kilipata fedha moja na shaba mbili.

Klabu ya Mathare Kaskazini ilipata fedha mbili pekee. Nayo Ruiru Prison ilipata dhahabu moja na shaba moja.

Kwa ujumla ni wachezaji 80 wa mchezo huo walioshiriki katika mashindano hayo ya siku mbili – Disemba 4 na 5 – katika ukumbi wa JKUAT, Juja, Kaunti ya Kiambu.

You can share this post!

CECIL ODONGO: Kauli ya Kalonzo na Mudavadi ithibati hawana...

MCAs waenda TZ kufunzwa adabu

T L