HabariKimataifa

ZIARA: Mkataba wa kibiashara baina ya Trump na Uhuru

August 28th, 2018 2 min read

NA PETER MBURU

RAIS Uhuru Kenyatta na Donald Trump wa Marekani Jumatatu walifanya mazungumzo ya kina kuhusu mbinu za kuimarisha biashara, uwekezaji na usalama baina ya mataifa yote mawili.

Katika kikao cha faragha kwenye Ikulu ya White House, viongozi hao walijadili namna wawekezaji kutoka US wataweza kufanya biashara humu nchini katika mazingira bora zaidi, bila kusumbuliwa.

Aidha, viongozi hao walijadili namna ya kuimarisha biashara ili kufaidi mataifa yote mawili, kwenye ushirikiano wa kisoko baina yao.

Walipofanya kikao na waandishi wa habari jijini Washington DC,  kabla ya mkutano wao, Rais Kenyatta na Rais Trump walieleza matumaini makuu kuwa watafikia maelewano yatakayoleta uthabiti katika sekta hizo.

“Kenya na Marekani zimekuwa na uhusiano thabiti tangu tupate uhuru, tuko hapa kuimarisha ushirikiano huo. Tumekuwa na ushirikiano mzuri haswa katika vita dhidi ya ugaidi,” akasema Rais Kenyatta.

Alisema idadi kubwa ya kampuni za US zinazofanya biashara Kenya zimesaidia katika maendeleo, akiongeza kuwa ziara hiyo itasaidia kuongeza na kuimarisha biashara yao.

“Tuko hapa kufuatilia na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara baina yetu ili kuona namna tunaweza kuinua tunapoendelea kwa nia ya kufaidi mataifa yetu,” Rais Kenyatta akasema.

Rais Trump aliahidi kutimiza ‘mazuri’ mengi baada ya mazungumzo hayo, mbali na kufanya miradi bora.

“Tunaenda kumalizia vitu vingi vizuri kwenye kikao hicho. Tutakuwa tukifanya dili nzuri kwa mataifa yote mawili,” akasema Rais Trump.

Mbeleni, Rais Kenyatta alikuwa ameshuhudia kutiwa saini kwa mikataba ya kibiashara, ambapo Kenya ilipata zaidi ya Sh23 bilioni kufadhili mradi wa umeme na chakula.

Wake za marais hao Bi Margaret Kenyatta na Bi Melania Trump vilevile walifanya kikao chao kujadili namna ya kuinua miradi wanayosimamia ya ‘Beyond Zero’ (wa Bi Kenyatta) na ‘Be Best’ (wa Bi Trump).

“Bi Kenyatta na Bi Trump walifanya kikao cha wazi kikihusisha malengo yao ya pamoja na miradi yao husika kuhusu watoto. Miradi yao imeungana katika kuinua na kulinda watoto,” ikasema habari kutoka ikulu ya White House.

Bi Trump anatarajiwa kuzuru Afrika Oktoba.