Habari MsetoSiasa

Ziara ya Moi yawakera wandani wa Ruto

June 19th, 2018 2 min read

Na ANITA CHEPKOECH

ZIARA ya kisiri ya Seneta wa Baringo Gideon Moi katika Kaunti ya Kericho imezua joto la kisiasa katika eneo la Bonde la Ufa na kuwakera wandani wa Naibu wa Rais William Ruto.

Wafuasi wa Bw Ruto walielezea kukerwa kwao baada ya picha kuchipuza katika mitandao ya kijamii ikionyesha Bw Moi akiwa na mwenyeji wake Gavana Paul Kipkwony katika Kituo cha Ustawishaji Vijana cha Chebwagan wilayani Bureti, Jumapili.

Ziara hiyo ya kushtusha ilizua maoni mbalimbali huku wafuasi wa Bw Ruto wakihoji lengo la Seneta Moi na kushutumu Gavana Chepkwony kwa kuwa kibaraka cha Kanu katika eneo hilo.

Seneta Moi na Bw Ruto tayari wametangaza azma zao za kutaka kuwania urais 2022 na wamekuwa wakipigania kudhibiti siasa za Bonde la Ufa.

Eneo la Kusini mwa Bonde la Ufa ni ngome ya Jubilee kwa mujibu wa matokeo ya kura za uchaguzi wa 2013 na 2017.

Diwani wa Kapsoit Paul Chirchir alisema kuwa japo Katiba inaruhusu kila Mkenya kwenda popote na kushirikiana na yeyote, watu wa Kericho hawatakubali kuhusishwa na chama cha Kanu kinachoongozwa na Bw Moi.

“Tunataka kuelezea ulimwengu mzima kuwa watu wa eneo la Bonde la Ufa watatembea na Kirgit (fahali) hatua kwa hatua hadi mwisho,” akasema Bw Chirchir huku akimrejelea Bw Ruto.

“Hatutaruhusu kucheza mchezo wa pata-potea katika siasa. Hatutakubali kubadili msimamo wetu wa kisiasa kwa senti kidogo kutoka Kabarak,” akaongezea.

Mbunge wa Kipkelion Magharibi Hillary Kosgei alisema kuwa mkutano baina ya Seneta Moi na Gavana Chepkwony hakuwa na athari zozote za kisiasa kwani hawakushirikisha viongozi wengine kutoka eneo hilo.

“Tunachukulia mkutano huo kama wa kibinafsi kama vile sisi huona Bw Moi akipiga picha na Gavana wa Kirinyaga Bi Ann Waiguru na mwenzake wa Mombasa Hassan Joho.”

“Bw Gideon Moi hana ujasiri wa kusimama na kuomba kura kutoka kwa jamii ya Wakalenjin, anachofanya ni kupiga picha na kuzitia katika mitandao ya kijamii,” akasema Bw Kosgei.

Wafuasi wa Prof Chepkwony, hata hivyo, walisema kuwa mbali na Bw Gideon kuwa mwekezaji katika sekta ya majani chai pia ana uhuru wa kikatiba wa kwenda popote.

Gavana Chepkwony alisema Bw Moi alienda kumfariji kwa kumpoteza mjomba yake, Stephen Kerio, karani wa baraza la mji la zamani, aliyezikwa Jumamosi.

“Kwa sababu gavana alikuwa na mpango wa kuzuru kituo cha vijana ilibidi aandamane na Bw Moi,” akasema mmoja wa maafisa wanaosimamia mitandao ya kijamii ya Gavana.