Ziara ya Rais eneo la Magharibi yayumba

Ziara ya Rais eneo la Magharibi yayumba

BENSON AMADALA na SHABAN MAKOKHA

UTATA umezuka kuhusu ziara ambayo Rais Uhuru Kenyatta alitarajiwa kuanza leo katika eneo la Magharibi.

Kulingana na Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya na Waziri wa Mafuta na Madini, Bw John Munyes, Rais Kenyatta alikuwa amepangiwa kuwasili mjini Kakamega leo Jumapili.

Hata hivyo, kumekuwa na majibizano makali kati ya viongozi wa kisiasa katika eneo hilo kuhusu taratibu za kuwajumuisha viongozi wote kwenye ziara hiyo.

Wabunge kutoka eneo hilo wamekuwa wakitofautiana vikali kuhusu ziara hiyo.

Baadhi yao walitishia kuteka mipango na maandalizi ya ziara hiyo.

Wabunge hao wenye ghadhabu wanawalaumu magavana kwa kuwatenga kwenye mipango inayoendelea kumpokea rais.

“Kwa kuwa hii ni ziara ya serikali ya kitaifa kuhusu maendeleo, tutachukua maandalizi yake kwani usimamizi na uendeshaji wa miradi ya kitaifa ni jukumu letu. Magavana wana serikali zao, hivyo hawawezi kuchukua majukumu yetu,” akasema mbunge wa Lugari, Bw Ayub Savula.

Mkutano maalum wa viongozi uliopangiwa kufanyika Ijumaa kuhusu ziara hiyo haukufanyika, baada ya wabunge kusema hawakuwa wamefahamishwa kuhusu uwepo wake.

Gavana Oparanya alikuwa ameahidi kuandaa kikao cha viongozi kutoka eneo hilo kuwaleta pamoja ili kuondoa tofauti zilizopo baina yao.

Hata hivyo, wabunge wanasisitiza watachukua udhibiti za ziara hiyo kwani inahusu miradi ya kitaifa.

“Tutakutana jijini Nairobi wiki ijayo kujadiliana zaidi kuhusu ziara hiyo. Baadaye, tutawaalika magavana kujiunga nasi kabla ya kukutana na Rais kupanga ziara hiyo kikamilifu,” akasema Bw Savula.

Akaongeza: “Hatujali muda ambao Rais atachukua kabla ya kuzuru Magharibi. Tunaloshikilia ni kuwa lazima mipango inayoendeshwa imshirikishe kila mmoja. Wakati alizuru Nyanza, kiongozi wa ODM, Raila Odinga aliendesha mipango hiyo kwa kuwajumuisha viongozi wote,” alisema.

Akaongeza, “Ndivyo alivyofanya kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, wakati Rais alipozuru eneo la Ukambani. Vivyo hivyo, tutawashirikisha viongozi wetu Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula kwenye mipango hiyo.”

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wamesema hawatahudhuria mkutano huo wa Nairobi, wakieleza kuwa inatosha Rais kukutana na magavana na kupanga ziara hiyo.

Wabunge wanaowaunga mkono Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula walikuwa wametishia kususia ziara ya Rais Kenyatta, wakisisitiza viongozi hao hawakushirikishwa kwenye mipango ya maandalizi ya ziara hiyo.

Hata hivyo, mbunge maalum Godfrey Osotsi alipuuzilia mbali kauli hizo, akisema kuwa ziara ya Rais haipaswi kuingizwa siasa.

“Rais Kenyatta ndiye kiongozi wa nchi. Yuko huru kuzuru mahali popote nchini bila kuomba ruhusa kutoka kwa mtu yeyote. Ninaunga mkono juhudi zozote ambazo zinalenga kulistawisha eneo letu kimaendeleo,” akasema Bw Osotsi.

Alisema wale ambao wanapinga ziara ya Rais Kenyatta pia walisusia mkutano ulioitishwa na Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, ambaye ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa kuhusu Miradi ya Serikali.

Mkutano huo ulifanyika katika Taasisi ya Kukuza Mitaala Kenya (KICD), jijini Nairobi.

You can share this post!

Kysa Karengata: Corona imevuruga sekta ya spoti pakubwa

Kauli za Uhuru zatishia Raila