Habari za Kitaifa

Ziara ya Ruto Nyanza yalenga kura za Raila 2027


ZIARA ya Rais William Ruto katika ukanda wa Nyanza wiki hii imeibua matarajio mengi huku wengi wakifasiri kuwa ni mbinu ya kuteka eneo hilo kisiasa kuelekea kura ya 2027.

Rais atakuwa akitembelea Nyanza kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwa wandani wawili wa Kinara wa ODM Raila Odinga kwenye Baraza la Mawaziri.

Rais anatarajiwa kuwa na mapokezi mazuri katika eneo hilo ambalo ni ngome ya kisiasa ya Bw Odinga hasaa baada yake kubuni serikali jumuishi na kuonekana ameridhiana na waziri huyo mkuu wa zamani.

Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi na mwenzake wa Fedha John Mbadi ni wandani wawili wa Bw Odinga ambao waliteuliwa katika baraza la mawaziri.

Kwenye ziara yake Nyanza, kati ya miradi ambayo Rais Ruto anatarajiwa kuzindua ni ule wa kawi kwenye kisiwa cha Mageta, Kaunti ya Siaya. Mradi huo unatarajiwa utagharimu Sh232 milioni na utazinduliwa rasmi Ijumaa Agosti 26, 2024 na Rais Ruto.

Kwa mujibu wa Bw Wandayi, mradi huo unalenga kuhakikisha maeneo mengi yanafikiwa na umeme ili taifa lijitosheleze katika sekta ya kawi.
“Kwa mara ya kwanza katika historia, nusu za nyumba 1,744 kwenye kisiwa cha Mageta zitakuwa na umeme,” Bw Wandayi akasema katika mahojiano na Taifa Leo hapo Jumapili.

Mradi huo ambao tayari umekamilika na ulitekelezwa na Kampuni ya Kusambaza Umeme na Kawi Mashinani (REREC), kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia.

“Kuwa na umeme kutasaidia katika kuwahifadhi samaki wanaovuliwa Ziwa Viktoria kwenye fuo za Kuoyo, Magare, Mahanga, Mitundu, Sika na Wakawaka,” akaongeza Bw Wandayi.

Rais atatua Nyanza mnamo Jumatano kisha aanze ziara zake Migori, Homa Bay, Siaya kabla ya kumalizia Kisumu, Kaunti za Luo Nyanza.

Japo Ikulu bado haijitoa ratiba ya ziara hiyo, kiongozi wa nchi anatarajiwa kutangaza ufadhili kwa miradi mbalimbali na kutoa mwelekeo kuhusu miradi iliyokwama.

Kati ya miradi ambayo imekwama ni barabara ya Mamboleo-Miwani, mzunguko wa barabara ya Ahero na pia Bwawa la Soin-Koru.

Pia Rais Ruto anatarajiwa kuzungumzia mradi wa ujenzi wa Chuo cha Mafunzo kuhusu Uvuvi katika wadi ya Kabonyo Kanyagwal eneobunge la Nyando, Kisumu.

Mradi huo ulikuwa ugharimu Sh2.5 bilioni ambazo zilikuwa za mkopo kutoka benki ya Hungary na pia serikali ilichangia ujenzi wake.

Hadi sasa umekwama na hakuna chochote ambacho kimefanyika.

Alipozindua ujenzi wake mnamo Oktoba 6 mwaka wa 2023, Rais alisema ungekamilishwa kufikia mwezi wa nane mwaka huu lakini hilo halijafanyika.

Wakazi wamekuwa na shaka iwapo mradi huo utafanikiwa ikizingatiwa ardhi hiyo ilifunikwa na mafuriko mnamo Aprili 2024.

“Tunamtaka Rais ahakikishe kuwa mradi huu unakamilishwa kwa sababu utafungua eneo letu kimaendeleo. Hata barabara za kufika hapa ni duni na tunatarajia zitaimarishwa iwapo mradi huu utafanikiwa,” akasema Judith Auma, mkazi wa Kabonyo Kanyagwal kupitia mahojiano na Taifa Leo.

Mnamo Alhamisi, Rais atahudhuria hafla ya kumkaribisha nyumbani Waziri wa Hazina ya Kitaifa John Mbadi katika eneobunge la Suba Kusini, Kaunti ya Homa Bay.

Siku ya Ijumaa atakuwa katika eneo la Ugunja, Kaunti ya Siaya ambapo atahudhuria hafla ya kumkaribisha nyumbani Bw Wandayi.

Mikutano ya Rais Luo Nyanza itakuja wiki mbili tu baada ya kuzuru Kaunti za Kisii na Nyamira ambazo pia huwa ni ngome za chama cha ODM.

Ziara hiyo ya Rais imefasiriwa kuwa chambo cha kunyakua ngome za Raila ambaye ni dhahiri yupo katika kifua mbele kwenye kinyángányiro cha kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Uchaguzi wa AUC ni mnamo Februari 2025 na iwapo Bw Odinga atashinda wengi wanafasiri hatakuwa akimakinikia siasa za nchi.

Kabla ya kuelekea Nyanza Jumatano, siku ya Jumanne Rais atakuwa akiongoza hafla ya kuzindua rasmi kampeni za Raila za AUC.