Habari

Ziara ya Ruto yazua mauti

October 5th, 2020 2 min read

BENSON MATHEKA Na MWANGI MUIRURI

ZIARA ya Naibu Rais William Ruto Kaunti ya Murang’a, Jumapili ilisababisha mauti baada ya fujo kuzuka kati ya mirengo miwili ya chama tawala cha Jubilee.

Watu wawili walikufa wafuasi wake walipokabiliana na wale wa Rais Uhuru Kenyatta katika mji wa Kenol vijana walipojaribu kuzuia Dkt Ruto na wabunge wanachama wa vuguvugu la ‘Tangatanga’ kuhudhuria hafla ya kuchangia kanisa mjini Kenol, eneobunge la Kandara.

Haikubainika aliyetuma vijana hao kuzua ghasia hizo ambazo Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai alisema zilichochewa na wanasiasa.

“Tunahimiza wanasiasa wajiepushe na matamshi na vitendo vya uchochezi. Yeyote anayehusika na vitendo vilivyo kinyume cha sheria atachukuliwa hatua kali,” Bw Mutyambai alisema.

Alisema ameunda jopo la wapelelezi wa ngazi za juu kuchunguza kilichosababisha fujo hizo na kuuawa kwa watu wawili.

Fujo hizo zilijiri baada ya wiki ya malumbano makali na vitisho kati ya wafuasi wa Dkt Ruto na wale wa Rais Kenyatta yaliyoanza naibu rais alipovamia makao makuu ya Jubilee akiwa na washirika wake wa kisiasa.

Maafisa wa chama hicho, wakiwa na baraka za Rais Kenyatta, walimpiga marufuku kukanyaga ofisi hizo na kupendekeza avuliwe wadhifa wa naibu kiongozi wa chama wakidai anamdharau Rais.

Duru zilisema kwamba, mmoja wa waliouawa alikuwa miongoni mwa kundi la vijana waliokuwa wakinuia kuvuruga hafla ya Dkt Ruto katika kanisa la AIPCA Kenol.

Dkt Ruto amekuwa akitumia michango makanisani kupigia debe azima yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wafuasi wa Rais Kenyatta wamekuwa wakimlaumu kwa kuanza kampeni mapema kinyume na agizo la Rais Kenyatta.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Abu Makori, ghasia hizo huenda zilipangwa na mrengo mmoja wa chama cha Jubilee lakini wafuasi wa Dkt Ruto wakazitumia kuendeleza ajenda yao. “Kupitia kitendo kama hicho cha kijinga, watu wawili wamekufa na bado ni 2020. Wakenya wanafaa kuendesha siasa kwa ukomavu. Vijana msitumiwe vibaya,” alisema.

Kulingana na Naibu Kamishna wa Murang’a Kusini, Mawira Mungania, mtu huyo aliuawa na umati fujo zilipozuka mwendo wa saa 7.30 asubuhi.

Wandani wa Dkt Ruto wakiongozwa na mbunge wa Kandara, Alice Wahome walidai kwamba, vijana wa mrengo wa Kieleweke wa chama cha Jubilee waliwasili mjini Kenol kuanzia saa kumi na moja alfajiri wakiimba nyimbo za kumsifu Rais Kenyatta.

Wafuasi wa Dkt Ruto nao walikusanyika haraka na mji wa Kenol ukabadilika kuwa uwanja wa vita.

Mkuu wa polisi eneo la Muranga Kusini Anthony Keter alisema, waliouawa walinuia kuvuruga mkutano huo.

Dkt Ruto na wanasiasa zaidi ya 40 washirika wake, walifaulu kuhudhuria hafla hiyo na kusisitiza kuwa hakuna kitakachomzuia kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Walilaani fujo hizo na kusema hawatatishika kuendeleza siasa za walala hoi kote nchini.

Wafuasi wa Rais Kenyatta kaunti ya Murang’a walijitenga na fujo hizo na kuwataka vijana kutotumiwa kuzua ghasia.

Akijibu washirika wa Dkt Ruto waliodai alipanga ghasia hizo, Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Murang’a Sabina Chege alisema tukio linafaa kulaaniwa.

“Kabla ya kuninyooshea kidole cha lawama, kilichotendeka APCA Kenol mjini ni cha kuhuzunisha na ninakilaani. Kitendo hicho hakina uhusiano na Sabina Chege au Naibu Rais William Ruto. Sisi ni marafiki,” alisema.

Seneta wa Murang’a Irungu Kangata alisema fujo hizo hazingetokea kama wafuasi wa Dkt Ruto hawangeanza siasa za mapema.

“Komesheni vita vya ubabe, vinasababishia nchi shida nyingi na kuhatarisha maisha ya watu wasio na hatia,” alisema kupitia Twitter.