Michezo

Zibeni pengo la Auba’ kisawasawa – Arteta

January 17th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta amewataka vijana wake “wajitume” zaidi ili kujaza pengo lililoachwa baada ya kushindwa katika rufaa ya kuondoa marufuku ya mechi tatu dhidi ya Pierre-Emerick Aubameyang kufeli.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Gabon, ambaye alifungua ukurasa wa mabao katika sare ya 1-1 dhidi ya Crystal Palace mnamo Januari 11, alionyeshwa kadi ya njano kwa kuchezea visivyo Max Meyer, lakini adhabu ikabadilishwa kuwa kadi nyekundu baada ya video kuonyesha alimkanyaga vibaya sana mchezaji huyo.

Arsenal ilikata rufaa dhidi ya kutimuliwa kwa nahodha Aubameyang, lakini haikufanikiwa kushawishi wakuu kupunguza adhabu hiyo.

Mchezaji huyo wa zamani wa Borussia Dortmund amefungia Arsenal mabao 14 kati ya 29 iliyopata kwenye Ligi Kuu (EPL) msimu huu.

“Wachezaji hawana budi ila kufanya kazi maradufu,” alisema Arteta alipoulizwa Jumatano ikiwa pengo hilo ni pigo kwa timu yake.

“Unajua, mmoja wa wachezaji tegemeo anapokosekana, wachezaji waliopo wanafaa kujitwika majukumu yake. Nina uhakika kuwa wanapokosa kuchezeshwa, wanatamani kupata fursa kama hiyo na wanazungumza sana.

“Wakati wao wa kuzungumza uwanjani umewadia. Unapoingia uwanjani, toa mchango wa kuonekana kuonyesha kuwa pia wewe ni mzuri kama yeye ama bora kumzidi. Fursa sasa ndiyo hiyo.”

Arteta pia amepata pigo baada ya beki Sead Kolasinac kuumia.

Beki huyo wa pembeni kushoto huenda asishiriki mchuano wa hapo kesho dhidi ya Sheffield United uwanjani Emirates kutokana na jeraha la paja, huku pia beki wa pembeni kushoto Kieran Tierney na beki wa pembeni kulia Calum Chambers wakiwa mkekani kwa muda mrefu.

Arsenal yahusishwa na Stones

Arsenal imehusishwa na beki wa Manchester City, John Stones, ambaye Arteta aliwahi kufanya naye kazi uwanjani Etihad, lakini alisema hakuna mpango wa kutafuta Muingereza huyo.

“John ni mchezaji ninayependa na kufuata soka yake. Tulimsaini nilipokuwa Manchester City na kufanya naye kazi kwa miaka kadhaa na ninamfahamu vyema,” alisema.

“Ninapoangalia mabeki wa kati, ana sifa nyingi ninazopenda, lakini kwa bahati mbaya hatuna haja naye.”

Sheffield United na Arsenal zinashikilia nafasi ya sita na 10 kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza, mtawalia. Timu ya Sheffield, ambayo ilizaba Arsenal 1-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza mnamo Oktoba mwaka jana, iko alama saba nje ya mduara wa kuingia katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) nayo Arsenal iko alama saba kutoka maeneo hatari ya kutemwa.

Aubameyang atakosa mechi za ligi dhidi ya Sheffield (Januari 18) na Chelsea (Januari 21) na ile ya Kombe la FA dhidi ya Bournemouth (Januari 27).