Michezo

Zidane akana dai la kumdharau Bale

July 24th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

MADRID, UHISPANIA

KOCHA Zinedine Zidane amejitetea kufuatia madai kwamba anamdharau nyota Gareth Bale, huku akisisitiza kwamba mshambuliaji huyo wa Wales alipuuzwa kwa sababu hakutaka kucheza dhidi ya Bayern Munich.

“Sijadharau yeyote,” kocha huyo wa Real Madrid aliwaambia waandishi wa habari kabla ya mechi ya kirafiki dhidi ya Arsenal jijini Washington.

Akaongeza: “Klabu inashughulikia uhamiaji wake. Msinihusishe kamwe. Tulipocheza na Munich, Gareth hakucheza vizuri kwa sababu hakutaka kucheza mechi hiyo.”

Zidane aliongeza mawazo ya Bale kwa sasa yameelekea kwingineko na “hakutaka kucheza kwa sababu ya suala hilo.”

Baada ya kichapo cha 3-1 kutoka kwa Bayern Munich, Jumamosi, Zidane alisema Bale ataondoka klabuni wakati wowote. Kuondoka kwake kutawapa raha watu wengi….. ningependa aondoke sasa kwa sababu simhitaji kamwe.”

Ni matamshi ambayo yalimponza ajenti wa mchezaji huyo, Jonathan Barnett aliyesema ni matamshi yasiyofaa kwa mchezaji ambaye ameisaidia klabu hiyo kutwaa mataji.

Bale ambaye ana umri wa miaka 30 ameamua kuondoka baada ya kutoelewana na Zidane tangu kocha huyo arejee klabuni msimu uliopita, kwa mara ya pili.

Fununu

Hadi sasa, haijulikani anakoenda baada ya kukaa Bernabeu tangu 2013 akitokea Tottenham Hotspur, lakini kuna fununu kwamba huenda akayoyomea nchini China kujiunga na klabu moja ya ligi kuu ya taifa hilo.

Nyota huyo kwa sasa analipwa Sh2.5 bilioni kwa mwaka baada kutozwa ushuru, lakini amejiandaa kabisa kuondoka.

Wawili hao walirushiana lugha chafu msimu uliopita, baada ya kocha huyo raia wa Ufaransa kusema mbele ya waandishi wa habari kuwa Bale hana umuhimu wowote kwenye kikosi chake cha sasa.

Naye Bale alijibu mapigo kwa kusema hawezi kuondoka ndani ya kikosi hicho, yupo tayari kuchea gofu huku pesa zake zikiingia klabuni, kwa vile amebakisha miaka mitatu katika mkataba wake.

Kiungo Dani Caballos ni mchezaji mwingine anayetarajiwa kuagana na Real Madrid, huku kukiwa na uvumi kwamba anasubiriwa kujiunga na Arsenal. Tayari kocha Unai Emery alinukuliwa akisema mpango huo unakaribia kukamilika.