Bambika

Zifahamu skendo zote za P Diddy ambaye amekuwa akitrendi

May 31st, 2024 4 min read

NA SINDA MATIKO

YALIYOMKUTA nguli wa RnB, R Kelly ndio yanaonekana kuanza kumwandama rapa na mfanyabiashara bilionea wa Kimarekani P Diddy.

Kwa miezi kadhaa, Diddy mwenye umri wa miaka 54 amekuwa akitrendi kwa skendo mbalimbali.

Wiki mbili zilizopita, Diddy alitrendi tena baada ya video ya kamera za CCTV kuibuka inayomwonyesha akimshambulia kwa mateke mpenzi wake wa zamani staa mwanamuziki Cassie.

Kwa zaidi ya miaka 10, wawili hao walideti kwa kuachana na kurudiana hadi maji yalipozidi unga na wao kuamua kuachana kabisa 2018.

Lakini hii haikuwa skendo ya Diddy ya kwanza. Kwa zaidi ya miongo mitatu katika maisha yake ya ustaa, Diddy amehusishwa na skendo kibao kuanzia kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, unyanyasaji wa kijinsia kwa wapenzi wake, visanga vya fujo na hata kifo.

Kubwa hata zaidi, hakuna kisanga hata kimoja kilichompelekea Diddy kufungwa jela.

Baadhi ya skendo kubwa za rapa huyo mtatanishi zilizoishia kugonga vichwa vya habari katika vipindi tofauti kwenye maisha yake hizi hapa.

Ahusishwa na vifo vya watu tisa, 1991

Mwaka 1991 jina lake likiwa ndio limeanza kushika kasi, Diddy aliandaa tamasha la basketiboli lililowakusanya mastaa kadhaa.

Tamasha hilo lilifanyika katika ukumbi wa City College of New York. Ni ukumbi uliokuwa na uwezo wa kupakia watu 2,730 lakini tamasha hilo liliishia kupakia zaidi ya watu 5,000 baada ya walinda usalama waliokuwepo kulemewa kudhibiti idadi hiyo kubwa ya watu waliotaka kuhudhuria.

Kwa kuhofia watu wangezidi zaidi, walinzi waliamua kufunga milango ya uwanja jambo lililopelekea kuzuka kwa msongamano wa watu waliong’ang’ania kuingia ndani kabla milango kufungika. Ni msongamano ulioishia kusababisha vifo vya watu tisa huku 29 wakijeruhiwa vibaya.

Diddy akashtumiwa kwa ukosefu wa kuajiri walinzi wa kutosha kwa ajili ya tamasha hilo lakini pia kuwapa vibarua walinzi chwara.

Diddy alijitoa kwenye ngori baada ya kukubali kuwafidia hela familia ya waliofiwa pamoja na waliojeruhiwa.

Amshambulia produsa studio 1998

Produsa na meneja wa rapa Nas (enzi hizo) Steve Stoute alikutwa na watu wawili wakiongozwa na Diddy ofisini mwake na kushushiwa kipigo cha mbwa kuingia msikitini.

Kosa la Stoute lilikuwa ni kutuma video ya wimbo wa Combs na Nas kwa stesheni ya runinga ya MTV bila ya kufuta kipande fulani ambacho Diddy (Combs) alikuwa amependekeza kifutwe.

Stoute alisema akiwa afisini mwake jinini New York, Combs na wapambe wake hao walimvamia kwa chupa ya pombe na kumwacha na majeraha ya usoni na mkononi.

Ni madai ambayo Diddy alikana mahakamani na kuomba radhi kwa kitendo chake. Hata hivyo, mahakama haikumpa kifungo baada yake kuridhia kumfidia Stoute.

Kisanga cha ufyatulianaji risasi kilabuni, 1999

Disemba 1999 Combs na wapambe wake walikuwa kwenye klabu ya Clabu New York wakijiachia. Uchokozi ukazuka baada ya Diddy kuigonga makusudi kinywaji cha jamaa mmoja Mathew Scar Allen.

Allen na Combs wakaanza kubishana. Allen, Combs na mpambe wa rapa huyo Shyne wote wakachomoa bastola zao na kuanza kufyatuliana. Watu watatu waliokuwemo klabuni wakaishia kujeruhiwa.

Combs na wenzake wakakamatwa huku rapa huyo akikutwa na bastola mbili ndani ya gari lake.

Alifunguliwa mashtaka ya matumizi mabaya ya bastola pamoja na hatia ya kutoa hongo baada ya kumhonga dereva wake kukiri kuwa bastola zile zilikuwa sio za Diddy ila za kwake mwenyewe dereva.

Hata hivyo, mahakamani Diddy alifutiwa mashtaka yote ila mpambe wake Shyne alihukumiwa kifungo cha miaka 10.

Azua sokomoko dhidi ya J Cole na Drake (2013, 2014)

Matukio yote yalihusiana na ugomvi wa nyimbo. Tukio la rapa J Cole lilitokea 2013 kwenye pati moja ya mastaa ambapo Diddy aliyekuwa amelewa kiasi cha haja alijaribu kumshambulia rapa Kendrick Lamar kisa vasi moja kwenye wimbo wake ambao Diddy alidai ulikuwa wakimchana yeye.

Rapa J Cole alipoona zogo likizuka, akaamua kuingilia kati kumsaidia rafiki yake Lamar na hapo akajikuta akikwaruzana na Diddy.

Kisa hicho kilifanikiwa kumalizwa chini ya maji ila baadaye J Cole alikuja kukiri kwamba yeye na Diddy walilimana mangumi kwenye pati hiyo iliyokuwa imeandaliwa na DJ Khaleed.

Mwaka uliofuatia Diddy aliripotiwa kumtandika ngumi ya usoni rapa Drake walipokutana kwenye klabu moja. Diddy alidaiwa kumsukumia konde nzito Drake baada yao kuzozana kuhusu wimbo fulani wa Drake. Hata hivyo, kwenye mahojiano ya baadaye Diddy alikana kumtandika Drake akisisitiza kuwa ni mshikaji wake yule.

Amtandika kocha wa soka shuleni alikosomea mwanawe, 2015

Juni 2015, Combs alihudhuria mazoezi ya soka ya timu ya shuleni UCLA alikosomea mwanawe Alosi.

Justin Combs alikuwa mmoja wa wachezaji waliounda kikosi hicho cha soka cha UCLA. Inadaiwa kuwa kocha Sal Alosi alimbeza Justin kwa kumtaka afahamu hatampendelea kwenye timu eti kwa sababu babake ni supastaa.

Baada ya mazoezi, Diddy alimfuata Alosi afisini mwake na kumshambulia. Diddy alikana kumshambulia akisema matukio yalivyoripotiwa kuhusu kisanga hicho hayakuwa sahihi.

Afisi ya wakili mkuu wa jiji la Los Angeles nayo iliamua kutomfungulia mashtaka Combs.

Ex wake Gina Huynh amshtumu kwa kumdhulumu kimapenzi, 2019

Baada ya kuachana na msanii Cassie 2018, Diddy alianzisha mahusiano na Gina ambayo yalidumu kwa miaka mitano.

Kwenye mahojiano, Gina alidai kuwa kwa miaka yote hiyo ya mahusiano, aliishi kunyanyaswa na kudhulumiwa kimapenzi na Diddy kubwa zaidi ikiwa ni kupigwa mara kwa mara.

Mrembo huyo alidai kwamba kuna nyakati Diddy alimtandika mateke ya tumboni kiasi cha kumpelekea kushindwa kupumua. Huu ndio ulikuwa utaratibu hadi alipoamua kujitoa.

Gina alidai mara nyingi aliposhushiwa kipigo na Diddy, alilinganishwa na Cassie huku rapa huyo akimpenda kumsifia sana Cassie.

Cassie amfungulia Diddy mashtaka ya kumdhulumu, 2023

Novemaba 2023 kabla ya video iliyovuja wiki mbili zilizopita, Cassie alimfungulia Diddy mashtaka kadhaa ya dhuluma za kimapenzi ikiwemo kisanga cha kumbaka 2018, kumtandika mara kwa mara, kumtishia maisha na kumlazimisha kushiriki mapenzi na wapambe wake huku yeye akitizama kama sinema.

Combs alikana mashtaka yote hayo na baadaye yeye na Cassie wakaafikiana fidia kwa ajili ya kudondosha kesi hiyo mahakamani.

Baada ya video akimtandika Cassie kuzuka inayomwonyesha pia akimgaragaza chini, Cassie aliandika posti akiomba watu kuwa wanaamini kwanza mapema mtu anapoibuka na madai ya kudhulumiwa, kwani yeye hakuhisi kama watu walimwamini mara ya kwanza alipoibuka na madai hayo hadi pale video ilipotokea ikidhibitisha lalama zake.

Hata baada ya kuzuka kwa video hiyo, afisi ya mwendesha mashtaka jijini Los Angeles ilisema haitamfungulia mashtaka Diddy maana matukio ya video hiyo yalitokea zamani kidogo na muda wa kufaili kesi kama hiyo kwa mujibu wa sheria ulikuwa umepita.