Makala

Ziko wapi Sh144m? Skendo ya Dishi na County yalipuka

May 3rd, 2024 2 min read

NA WINNIE ONYANDO

MPANGO wa Serikali ya Kaunti ya Nairobi kutoa chakula kwa wanafunzi, unaofahamika kama Dishi na County uliozinduliwa na Gavana Johnson Sakaja, sasa uko hatarini baada ya sakata ya ufujaji Sh144 milioni kulipuka.

Hii ni baada ya wasimamizi wa mpango huo kushindwa kueleza jinsi ambavyo mamilioni hayo ya fedha yalitumika.

Serikali ya kaunti hiyo imeshindwa kueleza jinsi ambavyo Sh144 milioni zilizotolewa na serikali ya Ufaransa kufadhili programu hiyo zilitumika.

Akiwa mbele ya Kamati ya Afya ya Bunge la Kaunti mnamo Jumanne, Waziri wa Afya wa Nairobi Susan Silantoi alisema kwamba serikali ya Gavana Sakaja haijaweka kanuni za kufuatilia jinsi pesa za Dishi na County zinavyotumika.

“Tuliwasilisha kanuni za kudhibiti matumizi ya fedha hizo kwa bunge mnamo Desemba 2023 lakini tukaambiwa zinapaswa kupitia kamati maalum kwanza. Kwa hivyo hadi sasa hazijaidhinishwa,” waziri Silantoi alisema.

Kamati ya Afya inaoongozwa na diwani Maurice Ochieng.

Pesa hizo za wafadhili zililipwa kwa Wakfu wa Food for Education, shirika ambalo linasimamia mpango wa Dishi na County katika kaunti mbalimbali.

Katika Kaunti ya Niarobi, serikali ya gavana Sakaja humlipia kila mtoto Sh25 huku wazazi wakilazimika kulipa Sh5.

Kwa upande mwingine, wafadhili na washirika wengine huchanga Sh15.

Naye Afisa Mkuu Mtendaji wa programu ya hiyo, Wawira Nyambura aliambia kamati hiyo kuwa Sh144 milioni zilipokelewa kama mchango kwa watoto 25,000 ambao hawana uwezo wa kulipa Sh5—pesa ambazo zinafaa kutolewa na wazazi.

Afisa Nyambura alisema shirika hilo hupokea michango kila siku kutoka kwa Wakenya na wafadhili wengine.

Hata hivyo, afisa huyo alishikilia kwamba hawawezi kutoa idadi kamili ya mchango waliopokea chini ya mradi huo.

Haya yanajiri miezi michache tu baada ya viongozi mbalimbali nchini akiwemo Mbunge wa Embakasi Mashariki Paul Ongili almaarufu Babu Owino kuukashifu mpango huo.

Mnamo Oktoba 2023, gavana Sakaja alimwakilisha Rais William Ruto kwenye Kongamano kuhusu Lishe Shuleni, ambalo lilifanyika nchini Ufaransa.

Mkutano huo uliwaleta pamoja viongozi mbalimbali wakiwemo marais na mawaziri.

Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kutoa changamoto kwa nchi mbalimbali kuwekeza katika mfumo endelevu wa lishe kupitia mpango kama vile lishe shuleni.

Mpango wa ‘Dishi na County’ unanuia kuwafaa wanafunzi 250,000 katika shule zote za umma jijini Nairobi.