Habari

Ziko wapi Sh30 bilioni makataa yakitimia Jumatatu?

September 28th, 2019 2 min read

Na PAUL WAFULA na BENSON MATHEKA

JUHUDI za Benki Kuu ya Kenya (CBK), za kutwaa mabilioni ya pesa zilizofichwa na mabwanyenye nyumbani kwa kuchapisha noti mpya na kuharamisha zile nzee za Sh1000 zimekosa kufaulu baadhi ya watu walipokosa kuzibadilisha noti hizo.

Makataa ya kubadilisha noti hizo ni Jumatatu na Benki Kuu ya Kenya wiki hii iliashiria kuwa haitaafikia malengo yake kikamilifu japo imetumia zaidi ya Sh15 bilioni kuendeleza kampeni ya kuwataka Wakenya kuzibadilisha noti hizo katika muda uliowekwa.

Kwa kukosa kubadilisha noti hizo, zaidi ya Sh30 bilioni zitakuwa karatasi kwa sababu baada ya Jumatatu, hazitaweza kutumika.

Katika shughuli hii, serikali ilitarajia kurejesha Sh217 bilioni katika uchumi ikiwa ni asilimia 80 ya pesa zote ilizosambaza nchini.

Hata hivyo, Gavana wa Benki Kuu ya Kenya Dkt Patrick Njoroge wiki hii alisema kufikia Septemba 1, ni watu 24 waliokuwa wamewasilisha Sh2 milioni katika benki zote 42 kote nchini.

Kulingana na Dkt Njoroge, asilimia 99 ya waliobadilisha noti, walikuwa na Sh1 milioni au chini tofauti na ilivyotarajiwa kuwa watu wangejitokeza kubadilisha mabunda ya pesa walizoficha nyumbani.

Hii inamaanisha kuwa huenda waliokuwa wameficha pesa hizo waliamua kuzibadilisha kwa Sh1 milioni au chini ya hizo ili kuepuka darubini ya CBK.

Pesa za ufisadi

Wadadisi wanasema huenda watu waliogopa kunaswa kufuatia kanuni kali ambazo CBK iliweka ili kuwanasa waliokiuka sheria au waliokuwa wakificha pesa za ufisadi.

Ingawa Dkt Njoroge anasema yaonekana hakuna watu waliokuwa wamehifadhi mabilioni ya pesa, wadadisi wanahoji ziliko noti ambazo hazikurudishwa huku ikadiriwa kuwa kutakuwa na pego la Sh30 bilioni iwapo noti hizo hazitarudishwa.

Mdadisi wa masuala ya uchumi, Tony Watima anasema kwamba kwa mfano ikiwa Sh20 bilioni hazitakuwa zimerejeshwa kufikia Jumatatu, uchumi wa Kenya utakuwa na upungufu wa Sh20 bilioni.

“Hii itaathiri uchumi,” asema.

Anasema CBK itahitajika kuchapisha noti zaidi ili kujaza pengo.

Hata hivyo, chama cha wamiliki wa benki (KBA) kinasema hakuna haja ya kuchapishwa kwa noti zaidi.

“CBK itakuwa imefahamu hasa kiwango cha pesa nchini na kwa kuisaidia kurekebisha rekodi zake,” alisema Afisa Mkuu Mtendaji wa chama hicho Habil Olaka.

Kulikuwa na hofu kwamba walioficha pesa hizo wangetumia mashirika ya kubadilisha pesa lakini Afisa Mkuu Mtendaji wa chama cha wamiliki wa mashirika hayo Mohammed Nur Ali alisema hilo halikutendeka.

“Hatukuona pesa nyingi ilivyotarajiwa. Nafikiri ni kwa sababu ya kanuni kali zilizowekwa. Ikiwa kufikia kesho pesa zilizoporwa hazitakuwa zimerudishwa, zitakuwa karatasi tu na hazitafaidi yeyote,” alisema Bw Nur.

Anasema inaamaanisha kwa watu wengi kushindwa kurudisha pesa hizo, ikiwa waliiba, shughuli hii imewatia doa.

Kulingana na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Watumiaji wa bidhaa nchini (Cofec-K), Bw Stephen Mutoro, CBK ilitumia pesa nyingi kwa shughuli ambayo haikufaulu ilivyotarajiwa.

“Ni wazi kuwa waporaji walianza kubadilisha noti kwa dola hata kabla ya serikali kuharamisha noti za Sh1000 na kuchapisha mpya,” alisema.

CBK imesema kuwa itatoa maelezo kuhusu hali halisi wiki ijayo.

Wadadisi wanasema ingawa CBK ililenga pia kupigana na noti feki za pesa, matapeli wameanza kughushi ilizotoa miezi minne iliyopita. Polisi wamekuwa wakinasa noti bandia za Sh100, Sh500 na Sh1000.