Habari MsetoSiasa

Zima kiburi, Tangatanga wamfokea Matiang'i

December 3rd, 2019 1 min read

WYCLIFF KIPSANG na TOM MATOKE

WANDANI wa Naibu Rais William Ruto kutoka Bonde la Ufa wametoa masharti makali ndiposa washiriki katika utekelezaji wa ripoti ya BBI.

Viongozi hao kutoka Kaunti ya Nandi wakiongozwa na Seneta Samson Cherargei na wabunge Julius Meli (Tindiret), Cornelius Serem (Aldai) na Wilson Kogo (Chesumei) wanataka Rais Uhuru Kenyatta kuagiza mawaziri kukoma kujihusisha na ripoti ya BBI.

Huku wakionekana kulenga Waziri wa Usalama Fred Matiang’i, wanasiasa hao walisema mawaziri hao wanasababisha mgawanyiko ndani ya chama cha Jubilee.

Seneta Cherargei alisema Rais Kenyatta na Dkt Ruto walipounda serikali baada ya uchaguzi wa 2013 na 2017 waliagiza mawaziri kujiepusha na siasa.

“Mgawanyiko uliomo ndani ya chama cha Jubilee hautaisha hivi karibuni endapo Rais Kenyatta hatatimua maafisa wakuu serikalini wanaojihusisha na siasa,” akasema Bw Cherargei.

“Mgawanyiko baina ya Rais Kenyatta na naibu wake unachochewa na mawaziri ambao wanataka kuhakikisha kuwa Dkt Ruto haingii ikulu 2022,” akasema Bw Serem.

Gavana wa Uasin Gishu Jackson Mandago na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen pia walimtaka Dkt Matiang’i kuheshimu viongozi waliochaguliwa na wananchi.

“Matiang’i ni lazima aheshimu viongozi waliochaguliwa na wananchi. Hatuwezi kuruhusu watumishi wa umma kama vile Matiang’i kuwa na ubaguzi katika kuwatumikia Wakenya,” akasema Bw Mandago.

Viongozi hao walishikilia kwamba masuala mengi yaliyomo ndani ya ripoti ya BBI yanaweza kutekelezwa kupitia bunge bila kura ya maamuzi.

Bw Murkomen alisema shughuli za serikali zinafaa kuendelea bila kutatizwa na kampeni za kutaka kufanyika kwa kura ya maamuzi inayoendeshwa wanasiasa wanaounga handisheki baina ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga..

“BBI ina mapendekezo mazuri ya kuboresha maisha ya Wakenya. Matiang’i aliteuliwa waziri kwa hisani ya chama cha Jubilee hivyo afanye kazi ya kuhudumia Wakenya,” akasema Mbunge wa Soy Caleb Kositany.