Kimataifa

Zimbabwe kutimua wafanyakazi 3,000 kuokoa uchumi

January 7th, 2019 1 min read

CHARLES WASONGA na MASHIRIKA

SERIKALI ya Zimbabwe imeanza mchakato wa kuwafuta kazi wafanyakazi 3,000 kutoka wizara yake ya vijana, huku ikijaribu kutimiza ahadi yake ya kupunguza idadi ya watumishi wa umma.

Hii ndio njia mojawapo ya serikali ya Rais Emmerson Mnangagwa  ya kufufua uchumi wa nchi hiyo iliyodororeshwa na uongozi mbaya wa mtangulizi wake, Robert Mugabe.

Mishahara ya watumishi wa umma huchukua zaidi ya asilimia 90 ya bajeti ya kitaifa ya Zimbabwe ambayo ni dola 4 bilioni za Amerika.

Taifa hilo haliwezi kumudu mzigo huo kulingana na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) ambayo inapanga kulikopesha pesa za kufufua uchumi wake na kuboresha maisha ya watu wake.

Kwenye taarifa, Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) ilisema kuwa ingepunguza maafisa 3,365 wa vijana katika Wizara ya Vijana, Michezo na Sanaa Januari 4, 2018. Hii ni kwa mujibu wa mapendekezo kwenye bajeti ya kitaifa iliyosomwa Novemba mwaka jana.

“Maafisa wa vijana watalipwa malimbikizi ya pesa zote wanazopasa kulipwa na zile za kabla ya notisi,” ikasema taarifa hiyo.

Rais Mnangagwa anakabiliwa na shinikizo za kutimiza ahadi yake ya kurekebisha uchumi ulioharibiwa katika enzi ya utawala wa Dkt Mugabe, ambaye alipinga mipango ya kupunguzwa kwa mishahara ya watumishi wa umma.

Hatimaye aling’olewa mamlakani na wanajeshi mnamo Novemba 21, 2017.

Hata hivyo, serikali inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa sarafu ya dola na nakisi (upungufu) katika bajeti ya kitaifa.

Taifa hilo ambalo huzalisha chakula kwa wingi pia imepoteza imani ya wawekezaji kutokana Afrika na mataifa ya ng’ambo.

Mnamo Oktoba baraza la mawaziri liliidhinisha mpango wa ufufuzi wa kiuchumi unaolenga kupunguza mzigo wa kulipa mishahara.

Vile vile, mpango huo unajumuisha kupunguzwa na matumizi ili kuisaidia taifa hilo kukamilisha mzigo madeni wa kima cha dola za Amerika bilioni 2. Haya ni miongoni masharti ambayo Zimbabwe iliwekewa na IMF kabla ya shirika hilo kuanza tena kuipa misaada ya kifedha.