Kimataifa

Zimbabwe ya pili Afrika kuhalalisha bangi

April 30th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

SERIKALI ya Zimbabwe imekuwa nchi ya pili barani Afrika kuhalalisha ukuzaji na matumizi ya bangi.

Gazeti la Herald, linalochapishwa nchini humo lilisema kwamba serikali imechapisha sheria ya kuhalalisha ukuzaji wa bangi.

Kulingana na gazeti hilo, kupanda bangi au mbanje inavyojulikana katika nchi hiyo, kutakuwa kwa utafiti na matumizi ya dawa. Zimbabwe imekuwa ikijadili kuhalalisha bangi kwa miezi minane iliyopita.

Wakuzaji, wasafirishaji na wauzaji wa bangi watakuwa wakipatiwa leseni ya miaka mitano chini ya sheria mpya.

Lesotho ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuhalalisha bangi Septemba mwaka 2017.

Polisi watakuwa na jukumu la kuhakikisha kwamba bangi inatumiwa kulingana na sheria na serikali inaweza kufanya mabadiliko kufuatia ushauri wa polisi.

Mjadala wa iwapo bangi inafaa kuhalalishwa umekuwa ukiendelea katika mataifa mengi barani Afrika.