Habari Mseto

Zingatieni usafi mkila mapochopocho ya Krismasi, wakazi waambiwa

December 20th, 2018 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

Serikali ya kaunti ya Nakuru imetoa onyo kwa wakazi kuzingatia usafi wakati wa sherehe za Krismasi ili kujiepusha na maradhi.

Kulingana na Idara ya Afya ya Umma, tahadhari hiyo inafaa kuzingatiwa pia wakati wa kuwachinja wanyama wakati wa sherehe hizo.

Afisa mkuu wa afya ya umma Bw Samuel King’ori alisema kuwa wakati wa sherehe za sikukuu, watu wengi husahau kuzingatia usafi na kuhatarisha maisha yao kwa njia mbalimbali.

“Wakati wananchi wanaposherehekea, tungewataka kuwachinja wanyama katika vichinjio vilivyo karibu ambako kutakuwa na maafisa wa afya wa kufanya ukaguzi,” alisema Bw King’ori.

Bw King’ori aliongeza kuwa, ulaji wa nyama ambayo haijakaguliwa kuna hatari kubwa kwani baadhi ya madhi yanayotokana na wanyama yanaua kwa haraka .

Alisema kuwa upishi wa chakula katika sehemu zilizo wazi pia unahatari zake na ni muhimu kuzingatia afya.

Kulingana na Bw King’ori, mji wa Nakuru uko katika barabara kuu na hivyo iko katika hatari ya kusambaza maradhi yanatokana na uchafu. Aliwataka wenye hoteli kujihadhari.