Michezo

Zizou alivyompokonya Mourinho tonge la Real

March 18th, 2019 2 min read

NA MASHIRIKA

JUMA lililopita, klabu ya Real Madrid ilimteua tena Zinedine Zidane kuwa kocha mpya wa klabu hiyo baada ya kumpiga kalamu Santiago Solari.

Zidane ambaye ni raia wa Ufaransa aliifunza Real Madrid hadi mwishoni mwa muhula uliopita na kuisaidia timu hiyo kushinda mataji ya Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA) kwa misimu mitatu mfululizo.

Sasa, amepewa mkataba wa miaka mitatu hadi mwishoni mwa 2022. Uongozi wa Real Madrid kupitia kwenye bodi ya klabu hiyo ulikutana juma lililopita na kumtimua Solari kwa kumweleza kwamba huduma zake hazikuitajika na kumkabidhi Zidane mikoba ya kuiongoza tena klabu hiyo.

Kocha wa zamani wa Manchester United, Jose Mourinho alikuwa amepigiwa upatu kupewa tena hatamu za kuiongoza Real Madrid na tangazo la yeye kupawa kazi lilitarajiwa kutolewa wakati wowote huku vyombo vingi vya habari duniani vikisoma habari hizo.

Kutangazwa kwa Zidane kuliwashangaza wengi, si kuhusu uwezo wake, bali nama alivyombwaga Mourinho ‘The Special One’ katika nafasi hii.

Mchuano huu ambao ulionekana kuelemea upande mmoja ukashindwa kwa urahisi.

Alipoulizwa namna alivyohisi baada ya kushindwa na limbukeni Zidane, Mourinho alisema hivi: “Mimi sijutii lolote. Hilo ni jambo zuri kwa Real. Kwa Zidane, ni wakati

wake mzuri kudhihirisha ubora wake. Na sasa akiwa na mradi mpya, ni jambo zuri sana.”

Real ilifanya uamuzi wa kumleta Zidane baada ya kubanduliwa nje katika kinyang’anyiro cha Klabu Bingwa Ulaya na limbukeni Ajax Amsterdam ambayo sasa itakutana na Juventus kwenye hatua ya robo fainali.

Aidha, kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Real imeachwa na Barcelona kwa pointi 12

huku tayari ikiwa imebanduliwa nje ya kivumbi cha Copa del Rey, yaani, taji la mfalme.

Hii ina maana kwamba, Real itamaliza msimu bila kombe lolote kabatini mwao.

Ule ushinde wa mabao 4-1 dhidi ya Ajax katika mtanange wa UEFA ulisababisha mashabiki wengi wa Real kuandamana nje ya uwanja wa Santiago Bernabeu ambapo walitaka Solari kutimuliwa na Mourinho kupawa nafasi ya kuongoza upya kikosi hicho.

Rais wa zamani wa Real, Roman Calderon aliambia jarida la Sky Sports juma lililopita kwamba wasimamizi wa klabu hiyo walikuwa wanamtaka sana Mourinho kukabidhiwa mikoba ila baadhi ya wachezaji kama vile nahodha Sergio Ramos, Karim Benzema na Marcelo wakamkataa kabisa Mourinho.

Mourinho alipoulizwa kama Real ilimfafanulia ni kwa nini aliachwa na nafasi yake kupewa Zidane alisema, “Mbona wanipe ufafanuzi?”

Ingawa Zidane amempiku Mourinho na kupewa hatamu za kuiongoza Real, bado anashutumiwa na baadhi ya wachanganuzi kwamba licha ya kushinda mataji ya UEFA mara tatu mfululizo, hakufanya vizuri kwenye kampeni za La Liga.

Huu utakuwa mtego mkubwa kwake na huenda ukaamua kama siku za usoni atapata nafasi ya kufundisha timu kubwa au ndio utakuwa mwisho wake kabisa katika taaluma ya ukufunzi wa soka. Kwa Mourinho ‘The Special One’, itabidi amejaribu tena bahati yake siku nyingine kwani kwa hili, Zidane amepiga 2-0!