Michezo

Zogo la familia ya kichuna laahirisha harusi ya Gareth Bale

July 30th, 2018 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

NYOTA wa Real Madrid na timu ya taifa ya Wales, Gareth Bale ameahirisha tena harusi yake na kichuna Emma Rhys-Jones hadi Agosti 2019 baada ya kuibuka kwa mtafaruku mkubwa katika familia ya wakwe zake watarajiwa.

Awali, harusi hiyo ilikuwa iandaliwe jijini Turin, Italia mwezi ujao huku mwanamuziki maarufu mzawa wa Amerika, Beyonce Knowles-Carter, 36, akitarajiwa kuwatumbuiza wageni katika hafla hiyo kwa kima cha Sh220 milioni.

Akihojiwa na gazeti la The Sun wiki jana, Emma, 26, alikiri kwamba kuahirishwa kwa sherehe hizo kutampa muda wa kuipatanisha famalia yake na pia kumwezesha kujiweka katika umbo sawa baada ya kujifungua majuzi.

Mnamo Juni 2018, Emma alimpa baba yake, Martin, 54, ilani ya kutohudhuria kabisa harusi yake wakati atakapofunga pingu za maisha na Bale, 29.

Hatua hiyo ya Emma ambaye ni mama wa watoto watatu ilichochewa na ufichuzi kwamba Martin, aliyewahi kufungwa jela kwa makosa ya ulaghai na utapeli, alikuwa akilimenya tunda bichi la kidosho Alina Baranova, 29.

Kwa mujibu wa Emma, hakuna jambo la aibu zaidi kuliko hilo la baba yake kuchovya asali kwenye mzinga wa kichuna ambaye kiumri, ana nusu ya miaka ya dume hilo.

Hadi kufikia sasa, Emma na Bale wamejaliwa watoto watatu – Alba Violet, 5, Nava Valentina mwenye umri wa miaka 2 na Axel Charles aliyezaliwa mwishoni mwa Mei, 2018.

“Si kitambo sana tangu Martin atoke jela baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka sita kwa kosa la utapeli wa zaidi ya Sh290 milioni nchini Marekani. Hatua yake ya kujinasia penzi la Alina ambaye ni muuzaji wa maua, ilimtia Emma aibu kubwa. Isitoshe, kimaadili, huyo ni demu ambaye Martin anastahili kumwita mtoto wake” akaandika msemaji wa familia ya Bale.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, Martin alikuwa amepanga kutumia harusi ya mwanawe kama jukwaa la kumtambulisha rasmi Alina kwa familia yake. Mfanyabiashara huyo aliyemtema mkewe (mamaye Emma), Suzzane mnamo 2005, amekuwa akitoka kimapenzi na Alina kisiri kwa miezi mitano iliyopita.

Wengine ambao Emma aliwakataza kuhudhuria harusi yake baada ya kutuhumiwa kuwa walanguzi wa dawa za kulevya, wezi wa saa za thamani kubwa na waporaji wa zaidi ya Sh110 milioni ni binamu yake Epiphany Dring, 29, shangazi yake Jane Nurns, 56, Carl Dring ambaye ni babaye Epiphany na mume wa shangaziye, Daniel, 42.

Emma na Bale sasa wanapanga kurasimisha uhusiano wao wa kimapenzi mnamo Agosti mwakani kupitia sherehe kubwa za harusi zitazoandaliwa jijini Cardiff, Wales.

Gazeti la The Sun linaarifu kwamba harusi ya wawili hawa ambayo iliahirishwa tena mnamo Aprili 2017 inapigiwa upatu kufikia kiwango cha ile iliyomshuhudia nyota Lionel Messi akifunga silisili za maisha na kidosho Antonella Ruccuzzo mnamo Juni 24, 2017.