Habari

Zogo la Malala, Oparanya kuhusu Mumias lachacha

June 7th, 2019 2 min read

Na SHABAN MAKOKHA

MZOZO kuhusu changamoto zinazoikumba kampuni ya sukari ya Mumias umechukua mkondo mpya baada ya Seneta wa Kakamega Cleophas Malala kudai Ijumaa kwamba Gavana Wycliff Oparanya alifuja Sh154 milioni zilizonuiwa kutumiwa kufufua kampuni hiyo.

Bw Malala alidai kuwa serikali ya kaunti hiyo ilibuni hazina maalum ya kufufua kampuni hiyo lakini pesa hizo hazikutumiwa.

“Nilipohudumu katika bunge la kwanza la Kaunti ya Kakamega kama diwani wa wadi ya Mahiakalo, tulitenga Sh200 milioni kwa hazina ya kufufua kampuni ya sukari ya Mumias. Leo hii ni Sh46 milioni pekee zilizosalia katika akaunti ya hazina hiyo. Nataka Gavana Oparanya atueleze ni nani aliyetoa Sh154 milioni na alizitumia kufanyia kazi gani kwa sababu pesa hizo hazikufika Mumias,” akasema Bw Malala.

Mwanasiasa huyo pia alimkosoa Gavana Oparanya kwa kuunda kamati ya watu 12 kuchunguza namna ya kufufua kampuni hiyo ya sukari.

Hii ni licha ya bodi ya wakurugenzi na wasimamizi kupinga hatua hiyo. Bw Malala alidai kuwa Gavana Oparanya hana mamlaka ya kubuni jopo kuchunguza matatizo katika sekta ya sukari hadi jopo kazi la kitaifa, ambalo anahudumu kama mmoja wa wenyekiti, litakapowasilisha ripoti yake kwa Rais Uhuru Kenyatta.

“Tunashangaa ni kwa nini Oparanya anaunda jopo lingine la watu 12 na kulitengea Sh10 milioni kwa kazi ambayo uhalali wake ni wa kutiliwa shaka,” akasema. Bw Malala aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha Amani National Congress (ANC), alimtaka Bw Oparanya kuelezea kilichosibu jopo-kazi la kufufua kampuni ya sukari ya Mumias alilobuni 2014 kabla ya kupendekeza kubuniwa kwa lingine.

“Nimechunguza bajeti ya ziada iliyowasilishwa katika bunge la kaunti na kugundua kuwa kamati hiyo ya watu 12 imepewa siku 14 kukamilisha kibarua hicho lakini ikatengewa Sh10 milioni. Nini mantiki ya hatua hii?” akauliza.

“Watu 12 wanawezaje kufanya kazi kwa siku 14 na kulipwa Sh10 milioni? Ni kazi gani wanayofanya kupokea malipo kiasi hicho. Mimi kama seneta ninapinga njama hii ya kufyonza pesa za umma bila sababu maalum,” akasema Bw Malala.

Jopokazi kutoa pendekezo

Jopokazi hilo linaloongozwa na Waziri wa Biashara, Viwanda na Utalii katika kaunti hiyo, Bw Kassim Were, linatarajiwa kupendekeza njia bora za kufufua kampuni hiyo ambayo inazongwa na mzigo mkubwa wa madeni.

Aidha, jopo hilo linatarajiwa kutambua na kupendekeza namna ya kulinda ardhi ya jamii katika eneo pana kunakozwa miwa kando na kulinda mali ya kampuni hiyo.