Habari

Zogo lanukia Ruto akitarajiwa katika mkutano wa BBI Meru

February 28th, 2020 2 min read

Na MWANDISHI WETU

ISHARA ya makabiliano katika mkutano wa Mpango wa Maridhiano (BBI) mjini Meru ilijitokeza Ijumaa baada ya uhasama baina ya mirengo ya ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’ kudhihiri.

Kwenye kongamano la wajumbe kutoka Mlima Kenya kabla ya mkutano huo wa Jumamosi, wabunge wanaomuunga mkono Naibu Rais, Dkt William Ruto walimsuta kiongozi wa ODM Raila Odinga wakidai anatumia muafaka kati yake na Rais Uhuru Kenyatta na mchakato wa BBI kuendeleza masilahi yake ya kibinafsi.

Wakiongozwa na Mbunge wa Chuka/Igambangombe Patrick Munene wabunge hao walisema Bw Odinga, ambaye alikuwepo, hakupaswa kuhudhuria mkutano huo ambao ulilenga kuandaa mapendekezo yatakayowasilishwa kwa jopokazi la BBI Jumamosi uwanjani Kinoru, Meru.

“Hatumtaki katika mkutano huu. Huu ni mkutano wa Mlima Kenya. Hatuwezi kuongea kuhusu umoja ikiwa Naibu Rais amefungiwa nje ya BBI,” Bw Munene alisema.

Hata hivyo, Bw Odinga alitetewa na Magavana wa Meru, Bw Kiraitu Murungi na Muthomi Njuki (Tharaka Nithi), Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya na Mbunge wa Kieni Kanini Kega.

Waziri Munya aliwakashifu wale ambao hawakumtaka Bw Odinga katika mkutano huo akisema unalenga kuwaunganisha Wakenya wote.

“Tunataka mabadiliko ya katiba ambayo yatahakikisha kila mtu anahisi kuwakilishwa serikalini. Tukome kuingiza maslahi ya kibinafsi katika mpango wa BBI. Sharti tuwe na mabadiliko yatakayonufaisha kila mmoja wetu,” Bw Munya akasema.

Naye Bw Kiraitu alisema kuwa Bw Odinga ni kiongozi wa kitaifa na ana haki ya kuhudhuria mkutano popote nchini Kenya.

“Wale ambao nia yao ni kuingiza siasa za pesa nane na mabishano ambayo hayana msingi ndio ambao hatutawaruhusu kuvuruga mkutano wetu kesho,” akasema.

Akiongea katika lugha ya Kikuyu, Mbunge wa Kieni, Bw Kanini Kega aliwahimiza wale wote ambao watahudhuria mkutano wa leo kudumisha amani na utulivu akisema “watu wa Mlima Kenya ni wapenda amani na hupenda kuwakaribisha wageni”.

Wiki jana, Dkt Ruto alitishia kukomesha mikutano ya BBI akisema inatumiwa na ODM kama majukwaa ya kueneza siasa za kupalilia chuki za kikabila nchini.

Lakini Bw Odinga anasisitiza kuwa mikutano hiyo ni wazi kwa kila mtu kwani na majukwaa ya kujadili masuala ya kuboresha taifa hili. Wiki jana wasaidizi wa Dkt Ruto walidokeza kuwa huenda akahudhuria mkutano wa leo, lakini kufikia jana haikuwa imethibitishwa ikiwa atafika.

“Ndio, Naibu Rais atahudhuria mkutano wa BBI katika kaunti ya Meru lakini Jubilee inajadiliana kuhusu suala hilo,” akasema naibu msemaji katika afisi ya Dkt Ruto Emmanuel Tallam.

Dkt Ruto amekuwa akifanya ziara nyingi katika eneo la Mlima Kenya hali ambayo imemfanya kupata uungwaji mkono kutoka kwa wabunge wengi wa eneo hilo.