Zogo lazuka kikao cha kutimua gavana

Zogo lazuka kikao cha kutimua gavana

NA DAVID MUCHUI

KIKAO cha kushirikisha umma kuhusu hatua ya kumtimua Gavana wa Meru, Kawira Mwangaza kilisitishwa mara kadhaa huku makundi hasimu yakikabiliana vikali katika Bunge la Kaunti hapo jana Jumatatu.

Wakazi wanaozidi 700 walijitokeza Jumatatu asubuhi kutoa maoni yao kuhusu mswada wa utimuaji utakaojadiliwa hapo kesho Jumatano.

Mawasilisho yanayozidi 100 yaliyoandikwa na kuwasilishwa huku wakazi wengine kutoka kila wadi wakiunga mkono mswada huo.

Kulingana na diwani wa Abogeta Magharibi, Dennis Kiogora, aliyewasilisha mswada huo, madiwani watakusanya maoni ya umma kabla ya mswada huo kujadiliwa kesho.

“Gavana atakuwa na muda wa kujitetea binafsi kupitia mawakili wake katika kikao hicho. Punde baada ya kusikiliza upande wake wa kujitetea na maoni ya umma, madiwani watachangia mswada. Madiwani watapiga kura kuhusu mswada huo wa kumtimua katika kikao cha adhuhuri,” alisema Bw Kiogora.

Kikao hicho cha umma kilivurugika wakati mkazi mmoja alipopinga mswada huo akihoji kwamba misingi inayotumiwa kwa utimuaji haina mashiko. Kambi hasimu zilikabiliana kwa malumbano makali huku kila upande ukijaribu kushinda mwingine na kusitisha shughuli katika bunge hilo.

Vurugu zilizuka wakati kundi linalopinga utimuaji huo lilipoingia kimabavu katika Bunge la Kaunti hiyo baada ya kuwashutumu maafisa wa Bunge la Kaunti hiyo kwa kuwazuia kuingia.

Wakazi wengi waliozungumza katika kikao hicho cha kushirikisha umma waliunga mkono utimuaji wakihoji kuwa gavana huyo amewakosea heshima viongozi wengine waliochaguliwa.

“Ikiwa gavana hawezi kufanya kazi na viongozi wengine waliochaguliwa, hastahili kuwa afisini. Ninaunga mkono mswada wa kumtimua,” alisema Bw Jackson Murithi, mkazi wa Muthara.

Bw David Thuranira kutoka wadi ya Mbeu alihoji kuwa gavana huyo hakuchaguliwa pekee yake wala hawezi kufanya kazi akiwa amejitenga.

“Gavana alipokuja katika wadi yetu, aliteua machifu wa kusimamia basari ya kaunti ilhali kuna kamati. Hii ni kinyume na sheria,” alisema Bw Japhet Iruki wa Wadi ya Mbeu.

Hata hivyo, Bw Samuel Kimathi kutoka Wadi ya Nkomo alisema hatua ya kumng’oa mamlakani gavana huyo haijatimiza wakati ufaao kwa sababu amekuwa afisini kwa muda wa miezi mitatu pekee.

“Viongozi wanafaa kuruhusu muda wa mazungumzo kwa sababu hatua ya kumng’atua gavana mamlakani itafanya maendeleo kukwama. Ni mapema mno kuhitimisha kuwa mvutano uliopo kati ya gavana na madiwani hauwezi ukasuluhishwa,” alisema Bw Kimathi.

Alitoa wito kwa Rais William Ruto kuingilia kati na kumaliza mivutano ya uongozi katika Kaunti ya in Meru.

“Kwa sababu chama cha UDA kina idadi kubwa ya madiwani Meru, tunamtarajia rais kuwaagiza waache mchakato huo wa utimuaji,” alisema.

Bi Eunice Gitonga alishutumu maafisa wa usalama katika bunge la kaunti nhiyo kwa kuwazuia wafuasi wa gavana kuingia katika kikao cha kushirikisha umma.

  • Tags

You can share this post!

BORESHA AFYA: Kwa afya ya akili

Kundi C: Argentina na Poland kukabiliana kesho Jumatano

T L