Dondoo

Zogo mke kuvukishwa mto na ‘ex’

December 11th, 2019 1 min read

Na Leah Makena

GACIONGO, THARAKA NITHI

Sinema ya bure ilishuhudiwa eneo hili mume alipompapura mke wake kwa kuvukishwa mto na mpenzi wake wa kitambo akishuku walikuwa na mpango wa kurudiana.

Mke wa polo alikuwa amejiunga na baadhi ya wanakijiji kuhudhuria sherehe ya kuhitimu kwa binamu yao mjini. Safari ilikuwa shwari ila walipokuwa wakirejea nyumbani wakafungiwa njia na mto uliokuwa umevunja kingo.

Wasafiri walilazimika kungoja kwa masaa kadhaa kabla ya mto huo kurejelea hali yake. Hata hivyo, hawakuwa na budi kulipa barobaro waliokuwa wakivukisha wasafiri na ndipo kidosho akapata ofa ya kuvukishwa bila malipo na mpenzi wa kitambo.

Baadhi ya waliojua kuwa jamaa huyo alikuwa akirushia kidosho mistari hapo awali walivutia polo waya na kumfahamisha yaliyokuwa yakijiri. Mume aliyekuwa dereva wa boda boda alifika hapo haraka upesi na kuzua kioja.

Aliposhindwa kukabili hasidi wake ambaye alipiga mbizi kwenye maji na kuvuka hadi ng’ambo ya pili, aligeukia mke wake na kumtandika akidai alikuwa mkosa heshima.

“Kati ya wanaume wote hawa huyo nyang’au ndiye umeona akuvukishe? Mbona basi hujapotea naye majini mkafufue uhusiano wenu? Hivi unataka kuonyesha watu hawa mimi sikufai? Nitakupa adabu leo,” polo alichemka.

Ilibidi wasafiri waingilie kati na kumnasua kidosho kutoka kwa mikono ya mume aliyelewa kwa hasira huku akimtaka kurejea kwa wazazi wake baada ya kukataa kuamini maelezo ya kidosho kuwa hawakuwa na uhusiano wowote kwa sasa.

Kidosho alisikika akisema hangerejea kwa polo tena licha ya wazazi wa pande zote mbili kufanya kikao cha kutatua mgogoro huo. Polo alitakiwa kuomba msamaha kwa kutandika mke hadharani.