Michezo

Zoo Kericho wapaa Leopards ikifufuka katika soka ya KPL

March 5th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

AFC Leopards pamoja na Zoo Kericho ndizo klabu zilizoimarika zaidi kwenye jedwali la Ligi Kuu baada ya mechi za raundi ya 16 kusakatwa wikendi iliyopita, huku Mathare United, Sofapaka na Nzoia Sugar pia zikipaa.

Mabingwa mara 13 Leopards maarufu Ingwe, walijiondoa katika nafasi ya 18 (mkiani) kwa kucharaza washindi wa mwaka 2006 SoNy Sugar 1-0 katika uwanja wao mpya wa nyumbani Bukhungu mjini Kakamega na kutulia nafasi ya 16.

Eugene Mukangula wa AFC Leopards ampita Moses Odhiambo wa Mount Kenya katika mchuano wa Ligi Kuu ya Kenya Februari 6, 2019, uwanjani Kenyatta, Machakos,Kenya. Picha/ Chris Omollo

Zoo ililemea wageni wake Posta Rangers 1-0 na kuimarika kutoka nambari 15 hadi 13.

Wafalme wa mwaka 2008 Mathare walikaba viongozi Bandari 0-0 mjini Mombasa na kutua katika nafasi ya pili.

Waliruka mabingwa watetezi Gor Mahia. Mabingwa wa mwaka 2009 Sofapaka wako juu nafasi moja hadi nambari nne. Walinyamazisha KCB.

Nzoia wameingia 10-bora baada ya kutwanga Tusker 1-0.

Bandari inasalia uongozini kwa alama 32 kutokana na mechi 15.

Mathare, ambayo imesakata mechi moja zaidi, imezoa alama 30. Gor, ambayo imeteremka nafasi moja hadi nambari tatu, imezoa alama 29 kutokana na mechi 14.

Sofapaka ina jumla ya alama 27 baada ya kucheza mechi 16.

Mabingwa mara 11 Tusker wanashikilia nafasi ya tano baada ya kuduwazwa na Nzoia na kushuka nafasi moja. Vichapo vitatu mfululizo vimehakikisha Tusker wanasalia na alama 25 kutokana na mechi 15.

Wako bega kwa bega na Kariobangi Sharks waliosalia nambari sita licha ya kukung’uta Chemelil Sugar 2-0.

Hakuna mabadiliko

Hakuna mabadiliko katika nafasi tatu zinazofuata zinazoshikiliwa na SoNy iliyolemewa na Ingwe, Western Stima iliyokabwa 1-1 dhidi ya Vihiga United, na Homeboyz iliyonyeshea Mount Kenya United magoli 6-0.

SoNy imejizolea alama 22 kutokana na mechi 16 nayo Stima ina idadi sawa ya alama, lakini imesakata mechi 15.

Homeboyz ina alama 21 kutokana na mechi 16.

Nzoia inafunga mduara wa 10-bora kwa alama 20 kutokana na mechi 15. Ulinzi, ambayo imetupwa chini nafasi moja hadi nambari 11, inasalia na alama 18 kutokana na mechi 15.

KCB haijasonga kutoka nafasi ya 12. Imezoa alama 16 kutokana na mechi 16. Ina alama moja zaidi ya nambari 13 Zoo na nambari 14 Rangers zilizosakata mechi 16 kila mmoja.

Rangers ilishuka chini nafasi moja.

Chemelil pia imeteremka nafasi moja hadi nambari 15 kwa alama 14. Imecheza mechi 15. Ingwe imezoa alama 13. Vihiga, ambayo haina ushindi katika mechi 15 mfululizo, inasalia ya 17 kwa alama 12.

Inatofautiana na Mount Kenya iliyo mkiani kwa ubora wa magoli.

Mshambuliaji wa Homeboyz Allan Wanga anaongoza ufungaji wa mabao. Amecheka na nyavu mara nane.

Mganda Umaru Kasumba (Sofapaka) na Enosh Ochieng’ (Ulinzi) wamefunga saba.