Michezo

Zoo Youth kileleni baada ya kupiga vijana wa Bondo

April 3rd, 2019 1 min read

NA JOHN KIMWERE

KIKOSI cha Zoo Youth kilitwaa usukani wa mechi za Kundi B Ligi ya Taifa Daraja la Pili huku Transfoc FC ikiichoma Transmara Sugar kwa mabao 2-1 Ugani Kenyatta Stadium, mjini Kitale. Zoo Youth ilijiweka kifua mbele ilipovuna alama tatu bila jasho baada ya Bondo United kulegea. 

Transfoc na Transmara Sugar kila moja iliteremsha mchezo safi kabla ya wenyeji kuzoa pointi zote muhimu. Zoo Youth inaongoza kwa alama 24 sawa na Bungoma Superstars tofauti ikiwa idadi ya mabao.

Wachezaji wa Transfoc ya kocha, Peter Olukusa walibeba ufanisi huo kupitia Lucky Mweu na Jospeph Esinyoni waliotingia bao moja kila mmoja.

Naye Siriba Ocharo aliibuka bora alipofungia Transmara Sugar bao la kufuta mchozi. “Bila kipendeleo Transmara Sugar ni timu nzuri wala hakuna mteremko dimbani,” alisema meneja wa Transfoc, Pascal Wekesa na kudai wamepania kuendelez mtindo wa kugawa dozi dhidi ya wapinzani wao.

Nayo Raiply FC iliiranda Egerton University kwa mabao 3-2, Poror Mote ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya GFE 105, huku Kisumu Hotstars na APs Bomet kila moja ikiagana sare tasa mbele ya Vihiga Bullets na Silibwet FC mtawalia.