Habari za Kitaifa

Vijana ‘wakaba’ wabunge koo

Na SAMMY KIMATU June 24th, 2024 2 min read

MSWADA tata wa Fedha 2024/25, ambao unasubiri kupitishwa na wabunge au kuangushwa Jumanne, Juni 25 umeendelea kupokea mapingamizi kutoka kwa vijana, wakisema kuupitisha ni sawa na kuenda kinyume na mapenzi ya Wakenya.

Vijana sasa wanataka mswada huo kurambishwa sakafu, wakiteta kupitishwa kwake kutawaongezea mahangaiko.

Bili hiyo inayoendelea kuzua utata, huku mchipuko wa vijana wachanga nchini almaaurufu Gen Z wakiapa kuendeleza maandamano kuupinga, wiki jana ulipita awamu ya pili ishara ya huenda ukafua dafu.

Aidha, wanamtaka Rais William Ruto kuangazia masula ya vijana na akina mama jinsi alivyoahidi katika manifesto ya Kenya Kwanza na katika kampeni kabla ya kuchaguliwa 2022.

Akiongoza mkutano wa vijana na wanahabari katika hoteli moja jijini Nairobi Jumapili, Juni 23, 2024, kinara wa Youth Aspirants Movement (YAM), Bw Peter Osteen Ngui alisema maandamano yanayoendelea kote nchini yakiongozwa na Gen Z ni kwa mustakabali wa Katiba.

Kundi hilo linarai Dkt Ruto kuanzisha mipango ya kubuni nafasi za ajira hapa nchini, badala ya kuwaahidi kwamba anawatafutia kazi ng’ambo.

“Ni haki yetu kuandamana Kikatiba. Sisi Vijana hatuna silaha na tunashangaa ni kwa nini polisi wanaturushia vitoza machozi badala ya kutupa ulinzi,” Bw Osteen akasema.

Mwenyekiti Wa Youth Aspirants Movement (YAM) Peter Osteen Ngui almaarufu Tsunami (tatu kutoka kushoto) baada ya kikao na wanahabari Nairobi kuhusu mustakabali wa taifa na maandamano ya Gen Z dhidi ya Mswada Wa Fedha 2024. PICHA|SAMMY KIMATU

Kiongozi wa nchi, hata hivyo, Jumapili alionekana kusalimu umri akiahidi kufanya kikao na Gen Z aliomiminia sifa akiwataja kama vijana walioonyesha kuthamini demokrasia bila kuegemea misingi ya kikabila.

Kwa sababu ya ukosefu wa ajira, vijana wa kizazi cha sasa wanalalamikia kushindwa kugharamia mahitaji muhimu ya kimsingi, yakiwemo huduma za afya na hata kuanzisha familia – ndoa.

Bw David Njoroge ambaye ni Katibu Mkuu wa vuguvugu la YAM, aliomba vijana kujitokeza kwa wingi katika maandamano ya Jumanne.

Hali kadhalika, naibu mwenyekiti wa kundi hilo, Bi Nasra Oman alimkumbusha Rais Ruto na serikali yake kwamba vijana wametelekezwa kinyume na alivyowahidi katika kampeni zake kabla ya kushinda kiti cha urais.

“Mama Mboga na wanabodaboda hawajainuliwa kiuchumi jinsi rais ulivyotuahidi. Tafadhali, timiza ahadi zako,” akasema.

Vilevile, kundi hilo la vijana lilisisitiza umuhimu wa makanisa na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya kidini kuiombea Kenya pamoja na viongozi wake, ili nchi idumishe amani na umoja.

[email protected]