Habari Mseto

Mfumo wa kidijitali kurejesha shuleni wanafunzi wa chekechea Pokot Magharibi

Na OSCAR KAKAI July 2nd, 2024 1 min read

KARIBU wanafunzi 16,000 wa chekechea ambao husomea kwenye Manyatta katika maeneo kame Pokot Magharibi wamenufaika kupitia mpango wa mfumo wa kidijitali kutoka kwa wadau na serikali ya kaunti hiyo. 

Manyatta, ni majengo ya udongo na nyasi ambayo aghalabu hupatikana katika jamii zinazoishi maeneo kame nchini.

Mpango huo wa kutumia apu ya EIDU kwa njia ya simu, utasaidia wanafunzi kupata elimu ya kisasa hasa maeneo ya mashinani.

Hata hivyo, mpango huo unakumbwa na changamoto za ukosefu wa stima, sola mbovu, wizi na walimu kukosa maarifa kutumia vifaa hivyo.

Mpango huo unalenga kusaidia kuimarisha masomo kwa wanafunzi na kuinua kiwango cha elimu ambacho kiliathirika kutokana na visa vya ujangili baada ya shule nyingi kuvamiwa, walimu kufukuzwa hali iliyochangia masomo kutatizika.

Kulingana na mratibu wa masomo ya chekechea Pokot Magharibi, Joseph Tonyirwo mpango huo umeashiria dalili za wanafunzi kutamani kurejea shuleni.

“Mpango huu umesaidia kuhamasisha watoto kurejea shuleni,” alifafanua Bw Tonyirwo.

Afisa huyo, hata hivyo, anasikitika umekumbwa na changamoto kama vile ukosefu wa umeme katika baadhi ya shule.

Alisema kuwa mipango maalum imewekwa kuhakikisha kuwa vifaa hivyo vinafanya vyema.

“Vimeundwa kiasi cha kuwa vinahifadhi nguvu za kawi kwa muda mrefu,” akasema.

Walimu watepelekwa kupata mafunzo ya ziada kujua kuvitumia.

Aidha, Bw Tonyirwo alizitaka shule kuhakikisha zinalinda vifaa hivyo.

“Mpango huu utasaidia kukomesha visa vya wizi wa mifugo, ndoa za mapema na ukeketaji ambavyo vimeshamiri eneo hili,” alisema.

Amos Musonye afisa kutoka EIDU Kenya, alisema lengo la mpango huo ni kusaidia wanafunzi kupata elimu bora kupitia mfumo wa kidijitali.

Naye mwenyekiti wa walimu kutoka eneo la Masol, Solomon Lolpoita aliihimiza serikali kuwekeza kwa sola ili wanafunzi wasitatizike kukata kiu cha masomo kupitia vifaa hivyo nguvu za umeme zinapopotea.

[email protected]