Michezo

Omanyala aahidi Wakenya sapraizi Michezo ya Olimpiki


BINGWA wa Afrika na Jumuiya ya Madola mbio za mita 100, Ferdinand Omanyala ameahidi Wakenya maajabu kwenye Michezo ya Olimpiki itakayofanyika jijini Paris nchini Ufaransa mnamo Julai 26 hadi Agosti 11.

Omanyala anashikilia rekodi ya Afrika katika umbali huo baada ya kukamata nafasi ya pili kwenye riadha za Kip Keino Classic Continental Tour kwa sekunde 9.77 mwaka 2021.

Katika mahojiano jijini Nairobi, afisa huyo wa polisi alidokeza kuwa lengo ni kuandikisha kasi ya juu inapohitajika.

“Mwaka huu, hatutaki kumwaga mtama kuhusu matarajio yetu. Tutachukua kila mbio inavyokuja jinsi nilishangaza kwa kutimka 9.79 wakati wa mchujo wa timu ya taifa ya Olimpiki majuma mawili yaliyopita,” akaeleza Omanyala.

Mtimkaji huyo, 28, aliongeza: “Nataka iwe maajabu pia Olimpiki, lakini tunafanya kila kitu sawa. Ninafurahia jinsi msimu unaendelea.”

Omanyala anayetarajiwa kuelekea Uholanzi hapo Julai 5 kwa michezo ya FBK mjini Hengelo hapo Julai 7, alisema kuwa mwaka huu ni kufanya mashindano machache na mazoezi mengi na kutoiva wakati usiofaa.

“Mwaka jana, tulikuwa tayari kabisa kwa mashindano wakati usiofaa mwezi Machi na Aprili. Lakini mwaka huu tunataka kuandikisha kasi nzuri ya juu inapohitajika kwa hivyo msitarajie mengi kutoka kwangu, lakini pia tarajieni mengi,” akasema Omanyala.

Omanyala ni mmoja wa watimkaji watatu pekee katika mbio fupi waliofuzu kuwakilisha Kenya kwenye Olimpiki za mwaka huu.

Mbali na Omanyala kuna Zablon Ekwam na Wiseman Were watakaoshiriki mbio za mita 400 na mita 400 kuruka viunzi, mtawalia.

Wakimbiaji hao watatu walikuwa na kikao na wanahabari katika kambi yao ya mazoezi ugani Kasarani Annex jijini Nairobi hapo jana.

Wanatarajiwa kukita kambi ya mazoezi mjini Miramas nchini Ufaransa.

Zaidi ya Wakenya 80 wamejikatia tiketi ya kushiriki Olimpiki kutoka fani za riadha, raga ya wachezaji saba kila upande ya wanaume, voliboli ya wanawake, judo, uogeleaji na fencing.