Habari

Vijana wenye marungu walivyopita barabara za Eldoret wakisaka waliothubutu kuandamana

Na TITUS OMINDE June 28th, 2024 1 min read

VIJANA zaidi ya 300 walikusanyika katika makao makuu ya Kaunti ya Eldoret mapema Alhamisi asubuhi kabla ya kuanza kushika doria katika barabara za mji wa huo.

Katika kile walichokitaja kama ‘kulinda mji wao dhidi ya waandamanaji wenye vurugu’, vijana hao waliobeba marungu walizunguka barabarani wakiondoa mabaki ya mawe yaliyotumiwa wakati wa maandamano ya Jumanne ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024.

Kulikuwa na mkanganyiko huku baadhi ya wafanyabiashara wakifunga biashara zao kwa haraka wakihofia kuporwa, kama ilivyokuwa Jumanne.

Baadaye walikusanyika katika makao makuu ya kaunti ambapo walifanya mkutano huku polisi wa kupambana na ghasia wakitazama kwa mbali.

Malori mawili ya maafisa wa kijeshi yalikuwa yamefika katika uwanja wa kaunti lakini waliondoka muda mfupi.

Kulikuwa na uwepo mkubwa wa maafisa wa usalama katika mji huo ili kuepusha mzozo kati ya waandamanaji wanaopinga ushuru na wale wanaounga mkono Mswada wa Fedha.

Watu hao wenye silaha waliwapiga wale walioonekana kuchukua picha zao na kurekodi shughuli zao.

Makundi hayo, kulingana na wakazi, yalikuwa ya watu wageni mjini humo.

Mapema Jumatano wafuasi wa kundi hilo walitembea baadhi ya barabara za mji huo wakiimba nyimbo za kitamaduni na kufanya maombi ya kitamaduni, sawa na vilio vya vita na ibada za utakaso kufuatia maandamano ya siku ya Jumanne ambayo yalisababisha uharibifu wa majengo na uporaji wa mali.