Habari za Kitaifa

Maandamano: Polisi wamwagwa katikati ya jiji, barabara ziko shwari


MAAFISA wa polisi wanashika doria katikati ya jiji la Nairobi huku maandamano ya Gen Z kupinga Mswada wa Fedha 2024 yakitarajiwa.

Polisi walifika katika barabara za Kati ya jiji kuanzia saa kumi na moja alfajiri na kupangwa katika maeneo wanayokutania vijana kuanza maandamano ambayo yamekuwa ya amani.

Katika makutano ya barabara za Kimathi na Kenyatta Avenue lori polisi lilikita saa kumi na moja na nusu asubuhi huku maafisa wakionekana kulenga eneo na Nation Center ambapo waandamanaji wamekuwa wakikusanyika.

Barabara za jijini hazina shughuli nyingi kama kawaida ishara kuwa wafanyabiashara wanahofia kufungua biashara zao.

Kuna magari machache katikati ya jiji kinyume na kawaida ambao huwa ni vigumu kupata egesho.

Chama cha Wanasheria nchini (LSK) kikiongozwa na Rais Faith Odhiambo  kimewataka waandamanaji kutohusika na ghasia, uharibifu wa Mali, kuchokoza polisi na kutovamia majengo yanayolindwa.

Faith Odhiambo, kiongozi wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK)

“Tunatoa wito kwa wananchi wote kuwa waangalifu zaidi wakati huu. Wacha tuendelee kushiriki na kuwasiliana habari yoyote ambayo unaweza kuwa nayo ili kujua waliko wenzetu,” alisema.