Habari

Miradi iliyokwama Mlima Kenya sasa yaanza kutekelezwa


SERIKALI imeanza kutekeleza miradi ya kuunganisha stima ya kima cha Sh2.1 bilioni katika eneo la Mlima Kenya.

Kulingana na Mkurugenzi wa Bodi ya Shirika la Umeme maeneo ya mashambani (REREC) Mark Nderitu, miradi 322 itakamilika mwaka huu.

Akizungumza Alhamisi katika hospitali ya kaunti ndogo ya Kimbimbi kaunti ya Kirinyaga wakati wa kliniki ya macho bila malipo, Bw Nderitu alisema serikali inalenga kuweka stima katika nyumba 15,500 katika eneo hilo.

Kliniki hiyo ilifadhiliwa na REREC, Chama cha wasio na uwezo wa kuona Kenya na serikali ya Kaunti ya Kirinyaga.

Bw Nderitu alisema miradi hiyo itafaidi familia nyingi katika eneo hilo lenye wakazi wengi.

Alisema serikali imedhamiria kuweka stima katika nyumba za wakazi kuwawezesha kijamii na kiuchumi.

Kaunti ya Kirinyaga pekee ina miradi 20 ya aina hiyo ambayo itafaidi nyumba 1,250.

“Tunafadhili miradi hii chini ya mpango wa kusambaza umeme vijijini, tunataka kila nyumba iwe na nguvu za umeme,” alisema.

Naye Waziri wa Kaunti ya  Kirinyaga anayesimamia Huduma za Matibabu na Afya Dkt George Karoki alisema kaunti hiyo imeshirikiana na REREC kusaidia wakazi wanaougua maradhi mbalimbali ya macho.

Alisema kliniki hiyo ilivutia wagonjwa 1,500.

“Tumefanikiwa kuwafanyia upasuaji watu 36 waliokuwa na mtoto wa jicho huku wagonjwa wengine wakipatiwa matibabu ya magonjwa mbalimbali ya macho na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Dkt Karoki alisema kuwa wakazi wengi walikuwa wakiugua magonjwa ya macho na ndiyo maana kaunti hiyo imeanzisha kitengo cha kisasa cha macho katika eneo hilo.

Aliwashauri wenye matatizo ya macho kutembelea kitengo hicho kwa uchunguzi mapema ili kuepuka kupata upofu kabisa.