Jamvi La Siasa

Peter Kenneth: Ushuru wa juu wa Kenya Kwanza utawarudisha nyumbani

May 16th, 2024 4 min read

NA MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA mwaniaji wa urais mwaka 2013 Bw Peter Kenneth,58, amekuwa kimya kwa muda mrefu baada ya kuangukia pua katika uchaguzi wa 2017 na kuambulia patupu mwaka 2022 alipomezea mate nafasi ya mwaniaji mwenza wa Raila Odinga.

PK kama alivyozoeleka, husemwa kuwa na uwezo wa kurithi usemaji wa Mlima Kenya.

Mwaka 2017 aliwania ugavana Nairobi lakini akashindwa na Mike Mbuvi Sonko.

Mwaka wa 2022 aliwania wadhifa wa mgombeaji mwenza wa mwaniaji wa urais Bw Odinga katika mrengo wa Azimio La Umoja-One Kenya lakini kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua ndiye aliteuliwa.

Kwa sasa, Bw Kenneth amerejea tena katika soko la kisiasa akitifua kivumbi kutokana na semi zake.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, anafichua nia yake kamili ambapo kando na kujadiliana na Naibu Rais Rigathi Gachagua, amekuwa akishauriana na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Aliyekuwa mwaniaji wa urais mwaka 2013 Bw Peter Kenneth,58, ambaye pia aliwahi kuwa mbunge wa Gatanga. PICHA | MAKTABA

Swali:  Kwa sasa mjadala mkuu Mlima Kenya ni kongamano la Limuru III ambalo limepangwa Mei 17, 2024: Utahudhuria?

Jibu: Sitahudhuria kongamano hilo kwa kuwa waliolipanga hawajatimiza vigezo vya nia njema. Hawakuhusisha watu wote waliotakikana kushauriana nao kiasi kwamba linaonekana kuwa na taswira ya kuzua migongano ya kisiasa badala ya kuunganisha. Ni kama kongamano hilo ambalo limepangwa ni la kufika kwa jukwaa kupiga kelele tu kujiangazia kama watetezi lakini nia fiche ikiwa ni kujitangaza kama wagombeaji wa nyadhifa katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Swali: Ungekuwa wewe ndiye wa kupanga Limuru III tungeona mambo gani?

Jibu: Ningehusisha sekta zetu zote za Mlima Kenya. Wanasiasa wengi iwezekenavyo, wawekezaji na wazee wa kitamaduni. Tungekuwa na mada za kuonyesha kwamba hali yetu ya dharura kwa sasa sio siasa bali ni uchumi. Ningehakikisha kwamba Naibu Rais Rigathi Gachagua na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta wanahudhuria kongamano hilo kwa kuwa tofauti za wawili hao ndizo mgawanyiko wa Mlima Kenya. Kongamano bila hao wawili sio la kuangaziwa kama la kuunganisha Mlima Kenya bali ni la siasa tupu.

Swali: Ni masuala yapi ambayo ungeyapa kipaumbele katika Limuru III yako?

Jibu: Dharura yetu kuu ni kuhusu mfumo wa ushuru kwa sasa. Tumekabwa na utawala ambao hautaki kuona Mkenya wa kawaida akipata faida. Ni utawala ambao unataka tu kupiga watu kiboko cha ushuru. Rais William Ruto na serikali yake ya Kenya Kwanza ni sharti kutambua ushuru uliopitiliza hurudisha nyumbani serikali. Mimi nilifanya kazi katika kitengo cha mipango ya kitaifa na ambacho ni idara ndani ya Wizara ya Fedha. Ninahofia kwamba ushuru wa aina hii unaweza kuangusha uchumi wa wawekezaji na wa kitaifa. Mada yangu kuu ya Limuru III ingekuwa: ‘Mlima Kenya tumekataa utawala huu wa ushuru’.

Swali: Inasemekana kwamba umekuwa ukikutana na Naibu Rais Rigathi Gachagua: Ukweli?

Jibu: Sijakutana naye moja kwa moja lakini nimefikiwa na baadhi ya wandani wake wakiniomba nishirikiane naye katika kusaka umoja wa Mlima Kenya na pia kusaka mustakabali kuhusu kesho yetu kisiasa. Mimi ninamtambua kuwa yeye ndiye Naibu Rais na pia nampa heshima ya kuwa katika afisi hiyo. Tutakutana hivi karibuni lakini sio kujadiliana kuhusu siasa bali kuhusu uchumi unaohusu wenyeji na wakazi wa Mlima Kenya na athari mbovu za ushuru wa kunyonga utajiri. Sekta ambazo Rais Ruto analenga katika utawala wake ni zile ambazo ziko na umuhimu sana na utajiri wa Mlima Kenya. Bw Gachagua anafaa amwambie mkubwa wake kwamba Mlima haujafurahia sera zake.

Swali: Wewe unamtambua Dkt Ruto kama Rais halali wa Kenya?

Jibu: Hilo hata sio swali. Utakosaje kutambua Rais aliye mamlakani? Ndio tulishindana naye na ikaishia kuwa yeye ndiye alitawazwa. Yeye ndiye aliapishwa na ndiye amekuwa mamlakani kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa. Itakuwaje niseme simtambui? Jinsi alivyotushinda kuna shaka kubwa kwa mtazamo wangu lakini kwa kuwa taasisi husika na itifaki za kutuongoza ziliishia kuamua yeye ndiye Rais, hata iwe chungu, yeye ndiye aliye mamlakani kwa sasa. Ninachomuomba tu ni “Rais usituadhibu kwa ushuru usioeleweka.”

Swali: Utasaidiaje katika kuzima ‘tamaa’ hiyo ya ushuru wa makali kwa raia?

Jibu: Nitakuwa katika mstari wa mbele raia wakihanikiza sauti zao kulalamika. Dawa ya kupata rasilimali za kutekeleza sera za utawala sio kupitia kuongeza ushuru katika sekta za kijadi. Mbinu ni kupanua jumuia ya kutozwa ushuru. Mimi nitasisitizia utawala huu kupitia majukwaa mbalimbali kwamba unavyotufanyia si haki kamwe na hatutanyamaza tukiangamizwa. Ikibidi, nitasimama kama mpinzani wa moja kwa moja dhidi ya Rais Ruto katika awamu iliyosalia ya mkondo huu wake wa kwanza mamlakani

Swali: Wewe bado uko Azimio La Umoja-One Kenya Alliance?

Jibu: Azimio lilikuwa tu basi la wakati huo la kuwania nia ya utawala. Kawaida ya taifa hili, kila uchaguzi huwa na basi jipya la kuwania nalo nafasi. Ikiwa ni imani tuliyokuwa nayo kama wawaniaji wa Azimio, basi niko nayo. Lakini kwa sasa huwezi ukasema uko wapi kwa kuwa siasa hufuata mawimbi fulani na huenda hata utupate sisi na Ruto ndani ya Azimio 2027 au hata utupate United Democratic Alliance…siasa huwa hivyo. Lakini cha kuelewa kwa sasa ni kwamba tunasuka mbinu muafaka ya kuungana kama watu wa Mlima Kenya na wengine nje ya eneo letu kwa manufaa ya kujaribu kusaka ubora wa taifa hili katika chaguzi zijazo.

Swali: Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na Bi Karua bado ni wakubwa wako kisiasa Mlimani?

Jibu: Kwa sasa mkubwa wa siasa za Mlima Kenya ni Rais Ruto. Yeye ndiye alichaguliwa na watu wetu kwa kura nyingi. Kile kinanishinda ni imekuwaje anashabikia ushuru ambao kwa mtazano wangu unakandamiza licha ya kukumbatiwa kama mtoto wa eneo letu na wapigakura wetu. Bw Kenyatta alitekeleza yake na akaenda, yetu tu ni kumheshimu na kumuombea mema katika maisha yake. Kuhusu Bi Karua, nilimuunga mkono kikamilifu alipoteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga licha ya kwamba katika msasa wa vigezo, alikuwa wa tatu nyuma ya kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na mimi. Namheshimu hadi sasa na ninatambua uwezo wake pamoja na misimamo yake, mingine mikali ajabu. Lakini kwa sasa hakuna mkubwa wa mwingine kwa kuwa sote sasa ni ndugu na tuko katika mkondo wa kujipanga na kujipamba kuhusu siasa za kesho. Hata Bw Odinga kwa sasa unaona anajipamba. Ilivyo ni kwamba, kwa wakati huu la dharura ni kutetea Wakenya wasiangamizwe na huu ushuru wa juu ambao mara nyingi walafi serikalini hufakamia na hakuna uwajibikaji wa kuwafunga jela mafisadi hao.

[email protected]