Habari za Kitaifa

Uvamizi wa mbung’o na ugonjwa wa malale watishia utalii

May 30th, 2024 2 min read

NA JESSE CHENGE

UVAMIZI wa mbung’o na kusambaa kwa ugonjwa wa malale katika sehemu nyingi nchini sasa unatishia sekta ya utalii, mkurugenzi wa Baraza la Kitaifa la Kukabiliana na Mbung’o na maradhi ya Malale na Nagana (KENTTEC) Isaiah Kiteto amefichua.

Bw Kiteto akifichua hayo akiwa katika Kaunti ya Bungoma mnamo Jumanne wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Kilimo kabla ya sherehe za Madaraka Dei zinazotarajiwa kufanyika mnamo Juni 1, 2024.

Alikuwa ameandamana na Katibu wa Kilimo Paul Rono katika Chuo Kikuu cha Kibabii.

Bw Kiteto, ambaye anahusika na utafiti na udhibiti, alisema kwamba mbung’o husababisha ugonjwa wa nagana kwa mifugo na wanyamapori, na malale kwa binadamu.

Wanyamapori wanaoathirika zaidi ni vifaru.

Mtaalamu huyo, aidha, alibainisha kwamba mbung’o wameathiri sana wanyamapori katika mbuga na hifadhi.

Hii ni kwa sababu wanaweza kufyonza damu kwa urahisi kutoka kwa wanyamapori.

“Wanyamapori hawaathiriki sana na ugonjwa wa nagana, lakini kifaru huwa katika hatari kubwa. Jinsi tunavyojua vifaru ni wanyamapori walio hatarini kutoweka, sanasana vifaru weupe,” alisema Bw Kiteto.

Alisema kwamba hakuna mtalii anayependa kutembelea hifadhi au mbuga yenye mbung’o.

“Ikiwa mnyama ni mgonjwa na ugonjwa huo uwe ni nagana lakini usigundulike mapema, anaweza kufa,” alisema.

Kuhusu kilimo, alisema kwamba mbung’o pia huathiri uzalishaji wa mazao kwani katika maeneo yenye uvamizi wao, kilimo hakiendi sawa.

Hii ni kwa sababu kama ng’ombe ni mgonjwa, hata huwa hana nguvu ya kuburura jembe la kulimia wakati mkulima anatayarisha shamba.

“Maeneo yanayokumbwa zaidi na mbung’o katika Kaunti ya Bungoma ni maeneo ya Sirisia na Bumula na hii imeathiri uzalishaji wa mifugo,” akasema.

Mbinu za kutambua maeneo yenye uvamizi wa mbung’o huhusisha kuweka vitambaa vyeusi na vya bluu, rangi ambazo wanapenda.

Mtego wa mbung’o. PICHA | MAKTABA

Vilevile, wanasayansi hutumia kemikali kama acetone na phenol ambazo hutoa harufu kama ya mkojo na pumzi ya binadamu na wanyama na ambayo huwavutia mbung’o.

Kukabiliana na mbung’o, aliwashauri wakulima kutumia pampu sahihi za kupulizia dawa na kuwekea mifugo uzio kwa njia ya kitaalamu.

Aidha alisema mabadiliko ya tabianchi ambapo ukame huenea pia huchangia katika kuweka mazingira ambayo mbung’o hupenda.

“Kuna maeneo yaliyokuwa na baridi na joto la chini ambapo mbung’o hawangeweza kuishi lakini sasa mabadiliko ya tabianchi yamechangia ongezeko la joto hivyo maeneo yanayoathiriwa na mbung’o yanaongezeka,” alisema.

Afisa Mkuu Mtendaji wa KENTTEC ni Pamela Olet.

Maeneo mengine mbali na Bungoma yanayoathiriwa na mbung’o ni Kaunti ya Kwale.

Soma Pia: Serikali mbioni kuangamiza mbung’o waharibifu Kwale