Habari za Kitaifa

Wafanyabiashara sita washtakiwa kwa ulaghai wa shamba la Sh11bn

May 15th, 2024 1 min read

NA RICHARD MUNGUTI

WAFANYABIASHARA sita wameshtakiwa kuwalaghai wakulima hekta 452 zenye thamani ya Sh11 bilioni eneo la Mavoko katika Kaunti ya Machakos.

Mohamed Kuroyow, Mohamed Salat Ibrahim, Omar Khalif Adan, Adow Ahmed Mohamede, Jeremiah Mutisya Paul na Joseph Njue walishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi katika mahakama ya Milimani Rose Ndubi.

Wote sita walikabiliwa na shtaka la kula njama ya kuwalaghai wanachama wa kampuni ya Drumvale Farmer’s Cooperative Society shamba la hekta 452 la thamani ya Sh11 bilioni.

Kuroyow, Ibrahim, Adan, Mohamed na Mutisya walikana shtaka la kusajili shamba hilo kwa majina yao wakidai wao ndio wamiliki halisi.

Ulaghai huo, hakimu alielezwa, ulitekelezwa kati ya Septemba 13, 2018, na Januari 7, 2021.

Watano hao mahakama ilielezwa walijiandikishia shamba hilo kwa majina yao katika makao makuu ya Wizara ya Ardhi katika jengo la Ardhi House, Nairobi.

Shamba hilo ni Mavoko Block 12 No.IR204303 LR.8529/7 (usajili wa awali nambari 8529/1).

Watano hao Mohamed, Adan, Kuroyow, Mutisya na Ibrahim, walijifanya wao ndio wamiliki halisi wa shamba hilo.

Pia watano hao walikana shtaka la kukata hekta 141 za shamba hilo la hekta 452 na kuliandikisha kwa jina la Ganana Developers Limited.

Bi Ndubi alielezwa thamani ya shamba hilo la hekta 141 ni Sh3 bilioni.

Washtakiwa waliachiliwa kwa dhamana ya Sh10 milioni.

Kesi itasikilizwa Mei 30, 2024.