Habari Mseto

Aisha Jumwa: Kenya Kwanza inajichimbia kaburi Kilifi

June 10th, 2024 2 min read

NA MAUREEN ONGALA

WAZIRI wa Jinsia, Bi Aisha Jumwa, ameibua wasiwasi kwamba huenda wanasiasa wa Kilifi wanaoegemea upande wa Rais William Ruto wakakumbana na wakati mgumu kushawishi wapigakura kuwaunga mkono akidai kuwa eneo hilo limetengwa kimaendeleo.

Akizungumza wakati wa hamasa kuhusu mpango wa serikali wa maendeleo ya 2023-2027 mjini Kilifi, Bi Jumwa alisema inasikitisha kwamba viongozi wa Kenya Kwanza hawatakuwa na lolote la kuwaonyesha wapigakura mashinani endapo watatakiwa kuonyesha serikali ina mipango gani kwa wakazi katika miaka minne ijayo.

Bi Jumwa alikosoa kundi linaloshughulikia mpango huo kwa kutenga Kilifi katika miradi muhimu ya maendeleo itakayotekelezwa chini ya Ajenda ya Rais Ruto ya Mabadiliko ya Kiuchumi ya Bottom-Up (BETA).

“Wakati tunapitia ripoti niliona miundomsingi ya kilomita 6,000 kati ya mingine lakini katika mikoa mingine, wametaja miradi hasa.

“Unakuta daraja linajengwa, barabara hii…na nikawaambia unajua unapoenda Kilifi na kuna barabara ambazo tunajua tunazipenda sana lakini hazijaorodheshwa, itakuwaje?

“Kwa sababu tunaenda kuwaambia wananchi na wataenda mashinani kuona miradi inayotekelezwa na Rais ndani ya miaka minne lakini kama hakuna kitu kwetu basi hakuna haja ya kwenda,” alisema.

Kulingana na Bi Jumwa, kuna ukosefu wa miradi muhimu ya Kilifi katika mpango huo kwa wahusika lakini hakuna hatua iliyochukuliwa.

“Hata baada ya wao kuahidi kurudi kwa Wizara ya Fedha na kukagua miradi, kwa bahati mbaya hakuna chochote kwa Kilifi,” alisema.

Waziri huyo alitaja mradi wa eneo la viwanda ambao ulikuwa bado haujaanza Kilifi hata baada ya serikali ya kaunti kutenga maeneo ya utekelezaji wake.

Alisema kama viongozi wa Kilifi, walitarajia kuona utekelezaji wa miradi tofauti katika maeneo ambayo serikali ya kaunti imetoa ardhi kwa serikali ya kitaifa kwa madhumuni ya maendeleo.

“Isiwe kwamba kila wakati hakuna pesa, ni Kilifi ambayo tunaambiwa hakuna pesa, na hatusemi haya ili kubandikwa jina la wakabila,” aliongeza.

Waziri huyo wa Jinsia alisema serikali ya Kaunti ilitoa ardhi huko Kayafungo huko Kaloleni na Gongoni katika Kaunti Ndogo za Magarini kwa ajili ya ujenzi wa bustani za viwanda.

Bi Jumwa alisema serikali ya kitaifa pia haiko wazi kuhusu mgao wa fedha za kustawisha kilimo cha korosho na nazi ambazo ni za thamani kubwa kiuchumi kwa wakazi wa Kilifi.

Aidha, alisema serikali ya kitaifa imeshindwa kuzingatia ufugaji wa ng’ombe wa maziwa huko Kilifi ambapo kaunti hiyo ilikuwa na uwezo wa kuzalisha maziwa kwa sekta ya kibiashara, pamoja na sekta ya Uchumi wa Baharini.

Hata hivyo, alitoa wito kwa umma na viongozi kuachana na siasa ambazo zitadumaza maendeleo katika kaunti hiyo na kutaka ushirikiano na serikali ya kitaifa.