Michezo

Arteta aliyekosa kushindia Arsenal kombe lolote, aishia kutuzwa kocha bora msimu huu

May 30th, 2024 2 min read

MADRID, Uhispania

KIUNGO mahiri wa Real Madrid Jude Victor William Bellingham ametwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Ligi K uu ya Uhispania maarufu kama La Liga.

Hayo yalijiri huku kocha wa Arsenal Mikel Arteta akiteuliwa Kocha Bora wa Ligi Kuu (Ulaya) katika hafla iliyoandaliwa kwa udhamini wa shirika la michezo la Dubai Globe Soccer Awards jijini Sardinia, Italia mnamo Jumanne.

Washindi wengine katika hafla hiyo ya Italia walikuwa Kylian Mbappe wa PSG ambaye alistahiwa kama Mchezaji Bora barani Ulaya, kocha Xabi Alonso wa Bayer Leverkusen aliyetawazwa Kocha Bora (Ulaya) na Harry Kane wa Bayern Munich kama Mfungaji Bora wa ligi kuu ya Bundesliga na barani Uropa (36 na 7).

Bellingham, 20 ameifungia Real Madrid mabao 19 katika La Liga mbali na kusaidia kunyakua ubingwa wa ligi hiyo ya Uhispania kwa pengo la pointi 10. Real ilizoa alama 95 nayo Barcelona ikafuata kwa pointi 85.

Katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), nyota huyo alifungia Madrid mabao manne na kuisaidia kutinga fainali ya michuano hiyo yenye hadhi kubwa Duniani.

Kikosi hicho cha kocha mkongwe Carlo Ancelotti kitakutana na Borussia Dortmund Jumamosi usiku katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ugani Wembley, nchini Uingereza.

Kwenye kura za kuchagua Mchezaji Bora wa La Liga zilizopigwa na manahodha pamoja na jopo la wataalamu, Bellingham alimaliza mbele ya Vinicius Junnior pia wa Real Madrid, Antoine Griezmann wa Atletico Madrid, Artem Dovbyk (Girona) na Robert Lewandowski wa FC Barcelona.

Staa huyo kadhalika aliibuka Mwanasoka Bora wa ligi kuu ya Bundesliga nchini Ujerumani msimu wa 2022/2023 alipokuwa akichezea Borussia Dormund kabla ya kujiunga na Madrid katika mkataba wa miaka sita uliogharmu kitita cha Sh14.8 bilioni.

“Ningependa kuweka wakfu huu kwa wachezaji wenzangu, kamati ya kiufundi, na zaidi mashabiki wote wanaunga mkono klabu hii bora zaidi Duniani,” alisema kiungo huyo ambaye hakuhudhuria hafla ya kutoa tuzo hizo Jumanne kutokana na shughuli nyingi za kujiandaa kwa fainali ya Jumamosi.

Katika ngazi ya kimataifa, Bellingham amechezea timu ya taifa ya Uingereza mara 29, huku akijivunia mabao matatu.

Anatarajiwa kuchukuwa jukumu muhimu katika kikosi cha kocha Gareth Southgate wa timu ya taifa ya Uingereza wakati wa fainali za Euro 2024 nchini Ujerumnai kuanzani Juni 14.

Uingereza imepangiwa kuanza dhidi ya Serbia mjini Gelsenkirchen mnamo Juni 16.

Kuelekea katika fainali ya UEFA, Bellingham alisema amepokea ujumbe kutoka kwa rafiki zake wanaochezea timu nyingi wakimtakia kila la heri. Nyota hao alisema ni pamoja na Mwingereza mwenzake, Jodan Sancho anayechezea klabu ya Borussia Dortmund ambacho alikichezea hapo awali.

Alipoulizwa iwapo amezungmza na mchezaji yeyote wa Dortmund, Bellinghama alikubali akisema ni kadhaa akiwemo Sancho aliyemuaambia,

“Tukutana huko, miongoni mwa maneno mengine mengi.

“Jadon ni mtu ninayeheshimu tangu aliponipokea nikijiunga na Dortmund. Ni mtu mzuri sana. Alinisaidia sana.”

Sancho alirejea Dortmund mwezi Januari kwa mkopo akitokea Manchester United baada ya kuvurugana na kocha Erik ten Hag.

Walikuwa pamoja katika kikosi cha Southgate kilichoshiriki Euro 2020, lakini hajajumuisha katika kikosi kinachoelekea Ujerumani kucheza Euro 2024.

Kocha Arteta aliyehudhuria hafla ya Sardinia alitoa shukrani zake kwa watu wote waliomuunga mkono kwenye safari yake ya kujenga timu madhubuti katika kipindi cha miaka minne sasa.

“Ninawashukuru sana wachezaji, benchi ya ufundi na wadau wengine mbalimbali kwa kututia motisha. Tumekuwa tukijenga timu hii kwa miaka minne na hadi sasa kikosi chetu kina msisimko, ari, ghera na motisha ya kushinda mataji.

“Tunafahamu kuwa upo ushindani mkali lakini hatutakufa moyo. Tutapambana nao sana,” akasema Arteta aliyeongoza Arsenal kumaliza ya pili katika Ligi Kuu ya Uingereza.