Habari Mseto

Caroli Omondi akejeli ODM kwa kutishia kumvua ubunge


MBUNGE wa Suba Kusini Bw Caroli Omondi amekejeli chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kwa kutisha kumuondoa bungeni akisema hatua hiyo itafeli kama mipango ya hapo awali.

Mbunge huyo aliambia wapigakura wa eneo lake, kupuuza matamshi yaliyotolewa na chama hicho kwamba wanachama wake waliokwenda kinyume na matakwa ya chama watafukuzwa.

Bw Omondi alikejeli mipango ya kumpokonya wadhifa wake wa ubunge akisema chama hicho hakina msingi wa kisheria kutekeleza hatua hiyo.

Wakati huo huo, mfanyabiashara na mhisani wa Nakuru, Bw Maina Wakabura amehojiwa na wapelelezi katika ofisi za Mkurugenzi ya Uchunguzi wa Jinai eneo la Bonde la Ufa mjini Nakuru, kuhusiana na maandamano dhidi ya serikali.

Bw Wakambura aliitwa na akajiwasilisha katika afisi za DCI Jumanne jioni akiwa na wakili wake, akahojiwa na wapelelezi kwa takriban saa moja.

Bw Wakabura alithibitisha kwamba aliitwa na afisa wa upelelezi wa makosa ya jinai katika kaunti ndogo ya Nakuru Mashariki, Bw Samuel Ngeiywo, kuhusiana na uchunguzi kuhusu maandamano yanayoendelea nchini kote.

Kupitia kwa wakili wake Bw Collins Odungo, alisema kuwa mteja wake alikuwa akiheshimu wito aliopewa na maafisa wa upelelezi, unaomtaka kujiwasilisha katika makao makuu ili kurekodi taarifa.