Habari Mseto

Idadi ya Wakenya kuongezeka hadi 70 milioni licha ya changamoto za maisha

June 8th, 2024 1 min read

NA MARY WANGARI

IDADI ya Wakenya imekadiriwa kuongezeka hadi kufikia 70.2 milioni katika muda wa miongo miwili ijayo huku umri wa watu nchini ukizidi kubadilika kuelekea tabaka la ujana, ripoti mpya imeonyesha.

Kufikia 2030, idadi ya Wakenya imekadiriwa kuwa 57.8 na 70.2 milioni kufikia 2045 huku jamii zikizidi kuongezeka katika muda wa miaka 50-60 ijayo, licha ya idadi ya watoto wanaozaliwa kupungua.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa na Baraza la Kitaifa kuhusu Idadi ya Watu na Maendeleo Nchini (NCPD) inaashiria vilevile mabadiliko katika umri wa Wakenya huku taifa likiwa na idadi kubwa ya vijana katika miaka ya 20.

“Kubadilika kwa kasi kwa idadi ya watu ikiwa hakutaangaziwa au kusawazishwa na ukuaji wa mapato kunaweza kuzidisha changamoto za maendeleo. Jamii yenye idadi kubwa ya vijana inahitaji kufadhiliwa kikamilifu ili kuweza kukidhi mahitaji mbalimbali,” alisema Waziri Ndung’u, aliyemwakilisha Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi katika hafla hiyo.

Kulingana na Mkurugenzi wa NCPD, Mohamed Sheikh, idadi ya vijana, watu waliofikisha umri wa kufanya kazi, wanawake waliotimiza umri wa uzazi na wazee imeongezeka huku idadi ya watoto walio chini ya umri wa miaka 15 ikiendelea kupungua tangu 1999.

Idadi ya watu katika rika la miaka 0-14 ni ishara ya uchanga katika jamii ya taifa, anafafanua Dkt Sheikh.

Ripoti hiyo, hata hivyo, inafafanua kuwa, umri wa wanajamii una athari ya moja kwa moja ukuaji, uzalishaji na matumizi ya raslimali.

Mabadiliko na athari hizi zimefungamana na ukuaji kimaendeleo kwa sababu umri unaathiri tabia na mahitaji ya watu kijamii na kiuchumi.

Ili Kenya kunufaika kutokana na mabadiliko haya katika idadi na umri, serikali imeshauriwa kubuni na kutekeleza sera mwafaka kijamii na kiuchumi hususan katika afya na elimu.