Habari Mseto

Jamii ya Waluo ijiandae kushirikiana na Ruto 2027, Sang asema

May 14th, 2024 2 min read

NA VICTOR RABALLA

GAVANA wa Kaunti ya Nandi Stephen Sang Jumatatu alisema kuwa Rais William Ruto atashirikiana na uongozi wa jamii ya Waluo katika ukanda wa Nyanza kuunda serikali ijayo.

Bw Sang alihakikishia jamii hiyo kuwa hatua ya Rais William Ruto kuunga mkono azma ya kinara wa Upinzani Raila Odinga kutwaa wadhifa wa mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) haihusiani na siasa za Uchaguzi Mkuu wa 2027.

“Kama Mkenya, tunaamini kuwa Bw Odinga ana maono, dhamira na uwezo wa kuipeleka Afrika katika ngazi ya juu zaidi,” alisema.

Gavana huyo pia alisema kuwa Rais Ruto anaunga mkono azma ya kiongozi huyo wa Upinzani kutwaa wadhfa huo licha ya kuwa Bw Odinga kuwa mpinzani wake katika uchaguzi mkuu uliyopita.

Gavana huyo alikumbusha jamii ya Waluo kuwa Bw Odinga na Bw Ruto walifanya kazi pamoja katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007 na kuwataka viongozi wa chama cha ODM kufanya kazi na serikali ya Kenya Kwanza kwa manufaa ya Wakenya wote.

“Tunahitaji kufufua urafiki kati ya jamii za Waluo na Wakalenjin kwani, sote tunatoka katika kabila moja la Niloti na tunahitaji kufanya kazi pamoja ili kuipeleka Kenya mbele,” akasema Bw Sang.

Mshirika huyo wa karibu wa Rais Ruto aliwapongeza viongozi wa jamii ya Waluo katika eneo la Nyanza ambao wameonyesha nia ya kuunga mkono serikali ya Kenya Kwanza huku akiwahakikishia Wakenya kuwa hakuna jamii itakayobaguliwa.

“Lazima tuunde serikali pamoja katika uchaguzi wa mwaka wa 2027,” Bw Sang alisistiza.

Gavana huyo alisema haya katika kanisa la Kiangilikana Jimbo la Maseno Mashariki, Ahero wakati wa kuchangisha pesa kwa ajili ya kumuaga Askofu Joshua Owiti ambaye muda wake unakamilika Julai.

Bw Sang alidokeza kuwa uteuzi wa jamii ya Waluo katika nyadhifa kuu serikalini ni ishara kuwa Rais Ruto anatayarisha azma ya muhula wake wa mwisho uongozini.

“Urithi na ufanisi wa utawala ujao utaamuliwa na wataalamu na viongozi wengi kutoka eneo hili ambao wanafanya kazi bila kuchoka ili kuhakikisha kuwa serikali imetimiza ahadi zake kwa Wakenya,” alisema gavana huyo.

Seneta wa Kisumu, Prof Tom Ojienda kwa upande wake aliitaka serikali kukamilisha ujenzi wa bwawa la Koru-Soin lenye thamani ya Sh20 bilioni ili kukabiliana na tishio la mafuriko katika eneo la Nyando.