Habari za Kitaifa

Jeshi kuwanyima wanasiasa helikopta

May 31st, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Ulinzi Aden Duale sasa amefafanua kuwa Idara ya Jeshi (KDF) haitaruhusu helikopta zake kutumiwa katika shughuli za kisiasa bali zile za kudumisha usalama pekee.

Akiongea mnamo Jumatano usiku wakati wa mahojiano katika kipindi cha JKLive kwenye runinga ya Citizen, Bw Duale alisema ndege na mitambo mingine ya KDF inastahili kutumiwa kwa shughuli za kijeshi pekee.

“Sasa tumeweka sera katika KDF kwamba helikopta zetu hazitatumiwa tena na wanasiasa. Hatutaruhusu mienendo hii mibaya ya mali ya jeshi kutumika kwa shughuli zisizolandana na kazi ya usalama na ulinzi,” akasema Bw Duale.

Alieleza kuwa helikopta hizo zimetengwa kwa majukumu maalum kama vile kulinda nchi, kusafirisha wanajeshi na kuendesha operesheni za kiusalama.

Bw Duale alisisitiza kuwa sera hiyo mpya itatumika sio tu kwa helikopta za KDF bali kwa mali yote ya Idara ya Jeshi.

Waziri huyo alieleza kuwa yeye atakuwa akitumia mali ya KDF akiwa katika shughuli rasmi kama Waziri wa Ulinzi.

“Aidha, mwenzangu wa Usalama Kithure Kindiki ataruhusiwa kutumia helikopta za KDF akizuru maeneo yenye visa vya utovu wa usalama kama vile Kaskazini mwa Bonde la Ufa, msitu wa Boni miongoni mwa maeneo mengine hatari,” akasema.

Hata hivyo, Waziri huyo hakutaja nyakati ambapo Naibu Rais Rigathi Gachagua au mawaziri wengine wa Serikali ya Kitaifa wataruhusiwa kutumia helikopta au mitambo mingine ya KDF.

Tangazo la Duale limejiri kufuatia malalamishi kwamba wanasiasa wamekuwa wakitumia ndege za KDF kiholela pasina mpangilio wowote.

Kwa mfano, mnamo Mei 17, 2024, duru zilisema kuwa afisa mhusika wa Jeshi la Wanahewa alikataa kutoa kibali kwa maafisa kutoka Afisi ya Bw Gachagua, waliotaka Naibu Rais atumie helikopta ya KDF kusafiri hadi Bomet kwa shughuli ya kitaifa ya upanzi wa miti.

Maafisa kutoka afisi ya Naibu Rais waliambiwa kuwa “amri kutoka juu imetolewa kwamba ndege za KDF zisitumike kwa shughuli zisizo za kijeshi.”

Ilisemekana kuwa hatua hiyo ilimkera Bw Gachagua na kwamba ilikuwa mojawapo ya sababu za yeye kususia shughuli 11 rasmi za kiserikali kwa kipindi cha siku saba. Lakini mwenyewe alisema alikuwa kwa mfungo na maombi katika mlima.