Akili Mali

Kaka watatu walivyopaisha biashara ya ufugaji kuku hadi sasa wana kichinjio

June 4th, 2024 2 min read

NA SAMMY WAWERU

MWAKA wa 2018, ndugu watatu Siaya walileta pamoja mawazo yao jinsi watakavyokomboa kaunti yao kupitia ufugaji wa kuku.

Wazo hilo lilichochewa na jinsi soko la bidhaa za kuku, haswa mayai lilisheheni yale ya kutoka nchi jirani.

Kero hiyo iliyoathiri uzalishaji wa ndani kwa ndani, haikuwa inatatiza Kaunti ya Siaya pekee, ila eneo la Nyanza kwa jumla na Magharibi mwa Kenya.

Kaka hao waliishia kubuni Obwombe Enterprises Ltd, kampuni inayotamba katika mtandao wa uzalishaji bidhaa za kuku.

“Mayai kuagizwa kutoka nchi jirani, iliashiria upungufu wa bidhaa hii nasi tukaona mwanya wa biashara,” anasema Paul Oketch, Mkurugenzi wa Mikakati Obwombe Enterprises.

Operesheni, Oketch anadokeza kwamba ilianza rasmi 2019 kwa ufugaji wa kuku wa mayai yasiyo na nguvu za kiume (layers).

Kuku 16,000

Kufikia 2020, Kenya ilipokumbwa na janga la Covid-19, Obwombe Enterprises ilikuwa ikifuga hadi kuku 16, 000.

Tulikuwa tunauza kati ya kreti 140 hadi 150 za mayai kwa siku, Oketch anaelezea.

Februari 2021, walipanua mawazo zaidi na kuingilia ufugaji wa kuku wa kienyeji walioboreshwa.

“Tuliegemea kwa kuku wa mayai yenye nguvu za kiume, tukaondoa stoki ya wanaotaga yasiyo na nguvu za kiume,” anafafanua mfugaji huyo mkakamavu.

Shabaha ya mpanuko huo, Obwombe Enterprises ililenga kukuza jamii kupitia wakulima wanaofuga kuku.

Oketch anasema waliondokea mkondo ambao ulidhamiria kukuza kampuni pekee, na badala yake kuleta mabadiliko kwenye jamii.

Miaka mitatu baadaye, ndugu hao wana kila sababu ya kutabasamu kutokana na hatua walizopiga.

Katika kijiji cha Mutumbu, Gem, Siaya, na kilomita moja kutoka barabara kuu inayounganisha Kisumu na Busia, ni mradi huo.

Kando na vizimba kadhaa vya kuku waliokomaa kutaga mayai, wana viangulio maalum vya kuotesha mayai na kuyaangua vifaranga, na ofisi.

Isitoshe, Obwombe Enterprises, Oketch anaambia Akilimali kwamba ina kichinjio cha kisasa cha kuku, maendeleo yanayotokana na mchango wake kwa wakulima kutambuliwa na wafadhili.

“United States Agency for International Development (USAID) kupitia mradi wake, Kenya Crops and Dairy Market Systems (KCDMS), ilituinua kwa kutufadhili na viangulio na kufungua kichinjio”.

Hali kadhalika, walisaidiwa kukumbatia mfumo wa kidijitali kusajili wafugaji, kufuatilia utendakazi wao na idadi ya kuku wanaofuga, kutambua ikiwa wamekomaa na endapo wamepata chanjo.

Mradi huo hata hivyo ulikamilika 2023.

Wakati wa mahojiano Siaya, Oketch alidokeza kwamba data ya 2023 inaonyesha kuwa wanahudumu na wakulima wasiopungua 3, 800 kutoka Nyanza na Magharibi mwa Kenya.

Kutotesha mayai

Huwauzia vifaranga, na wengine kuwapa huduma za kuotesha mayai, kisha inanunua kuku wanapokomaa jambo linaloondolea wakulima mahangaiko ya kusaka soko.

“Mayai, tunanunua Sh25 kwa kila yai na kuku wanachezea kati ya Sh650 hadi Sh700,” Oketch anaelezea.

Kimsingi, Ombwombe Enterprises inaonekana kuzamia uongezaji thamani bidhaa za kuku; kuangua mayai kuwa vifaranga, ambao wakiuziwa wakulima, wanarudi kuwanunua wakiwa wamekomaa, na vilevile mayai.

Kuku huuzia walaji wakiwa wa nyama kati ya Sh800 hadi Sh850, na vifaranga wa siku moja hapungui Sh110.

Aidha, kampuni hiyo ina viangulio vya idadi jumla ya mayai 14, 000, kila baada ya siku 21.

Licha ya mafanikio yake, Oketch analalamikia gharama ya juu ya malisho haswa malighafi kuyaunda ambayo bei yake ni mithili ya dhahabu.

Isitoshe, anahisi idadi ya wakulima wanaohudumu nao ni wachache mno kufuatia upungufu wa mayai.

Wafugaji wamekuwa wakiteta kuhusu uhaba wa vifaranga nchini.