Habari za Kitaifa

Kampuni za ulinzi zavuna wenye biashara wakiwakimbilia kujikinga na waporaji

Na BARNABAS BII July 3rd, 2024 1 min read

KAMPUNI za ulinzi za kibinafsi zimeongeza ada za huduma zao kutokana na mahitaji makubwa kutoka kwa wafanyabiashara na kampuni zinazotaka kulinda mali maandamano yakiendelea kote nchini.

Biashara nyingi zimepata hasara ya mamilioni ya pesa baada ya maandamano yaliyochochewa na Mswada wa Fedha wa 2024 uliokataliwa na Rais William Ruto kugeuka kuwa fujo na uporaji katika maeneo mengi nchini. Biashara zimeporwa katika maeneo kama Nairobi, Mombasa, Nakuru na Eldoret.

Wamiliki wa biashara katikati mwa jiji la Nairobi Jumanne walijipanga na kujihami ili kulinda biashara zao dhidi ya waporaji, baada ya kupata hasara wiki jana.

Katika Kaunti ya Uasin Gishu wawekezaji wengi na wafanyabiashara wameajiri walinzi wa ziada wa kibinafsi ili kuimarisha usalama.

“Kuna ongezeko la mahitaji ya walinzi wa kibinafsi na wawekezaji wanaotaka kulinda mali yao dhidi ya uharibifu, iwapo machafuko yatatokea kama ya Jumanne iliyopita,” alisema Joshua Too, mhudumu wa kampuni ya usalama ya kibinafsi huko Eldoret.

Uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara wameacha kuhifadhi bidhaa kwa hofu ya kuporwa.