Habari za Kitaifa

Korti yazima polisi kutumia vitoa machozi na ukatili dhidi ya waandamanaji


MAHAKAMA Kuu Ijumaa Juni 28, 2024 ilitoa agizo la kuzuia polisi ya kitaifa kutumia maji ya kuwasha na vitoa machozi dhidi ya waandamanaji wanaodumisha amani.

Maafisa wa polisi waliamriwa kusimamisha matumizi ya risasi, risasi za mpira, silaha butu na hatua nyingine kali dhidi ya waandamanaji.

Mahakama Kuu pia iliagiza maafisa wa usalama wanaosimamia waandamanaji kuacha kutumia nguvu za kikatili au aina yoyote ya ghasia au  mauaji yoyote kinyume cha sheria.

Vile vile, Mahakama Kuu iliamuru polisi kusitisha kukamata watu kiholela, utekaji nyara, kuwekwa kizuizini, unyanyasaji, vitisho, ukatili, na udhalilishaji dhidi ya raia wanaoandamana kwa amani.

Mahakama ilitoa maagizo hayo kufuatia kesi iliyowasilishwa na Saitabao Ole Kanchory ambaye alitaka mahakama hiyo kuingilia kati kufuatia dhuluma za hivi majuzi zilizoshuhudiwa kote nchini.