Lugha, Fasihi na Elimu

KUCCPS: Wengi wapendelea shahada ya Elimu

May 21st, 2024 1 min read

NA MWANDISHI WETU

WATAHINIWA wengi wa Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE 2023) na wengine waliotuma maombi kwa elimu ya juu 2024-2025 walipendelea Shahada ya Elimu.

Afisa Mkuu Mtendaji wa KUCCPS Mercy Wahome alisema Jumanne kwamba anakadiria maombi zaidi ya 30,000 yalilenga kozi ya ualimu.

Akitoa ripoti kuhusu maombi hayo yaliyotumwa kati ya Februari 7, 2024, na kukamilika mnamo Machi 4, 2024, Bi Wahome alisema KUCCPS ilipokea maombi kutoka kwa watahiniwa 899,232 kung’ang’ania nafasi 1,078,806 katika vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu, zikiwemo za kozi za kiufundi.

Ripoti hiyo ilitolewa katika ukumbi wa Edge Convention Centre jijini Nairobi.

Watahiniwa 153,274 wa KCSE 2023 kati ya 201,146 waliopata alama za kuwawezesha kujiunga na vyuo vikuu, wamepata nafasi kufanya kozi mbalimbali.