Habari za Kaunti

Kucheleweshwa fidia ndio chanzo cha mikosi katika ujenzi wa barabara – Wazee

February 22nd, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

WAZEE kutoka jamii ya walio wachache ya Waboni, Kaunti ya Lamu sasa inadai kucheleweshwa kwa fidia ya vipande vyao vya ardhi iliyotwaliwa na serikali kwa ujenzi wa barabara kuu ya Lamu-Ijara-Garissa ndio chanzo kikuu cha mikosi inayoshuhudiwa kila mara katika mradi huo.

Ujenzi wa barabara hiyo ya kima cha Sh17.9 bilioni, ambayo ni kiunganishi kikuu cha Kenya kupitia Bandari ya Lamu na Miundomsingi ya Uchukuzi ya nchi jirani za Sudan Kusini na Ethiopia (Lapsset), ulizinduliwa na kuanzishwa rasmi mnamo Aprili 2021.

Mradi huo ulipangiwa kukamilika baada ya miaka miwili, kipindi ambacho kilifaa kukamilika mwezi Mei, 2023.

Mradi huo hata hivyo umekuwa ukiandamwa na mikosi tele, ikiwemo mashambulio na mauaji ya kila mara ya kigaidi kutoka kwa Al-Shabaab yanayolenga hasa wajenzi na wasimamizi wa mradi, hivyo kulazimu kazi kusitishwa mara kwa mara.

Katika mahojiano na Taifa Leo Jumatano, wazee wa jamii ya Waboni ililalamikia hatua ya serikali ya kuwafurusha kutoka kwa makazi na mashamba yao kwa kigezo kuwa ingewafidia, ahadi ambayo hadi sasa haijatimizwa.

Barabara hiyo ya Lamu-Ijara-Garissa inapitia au kupasua katikati ya msitu mkuu wa Boni ambao ndio ngome kuu ya jamii ya walio wachache ya Waboni.

Vijiji vyote karibu sita vya Waboni, ikiwemo Milimani, Basuba, Mangai, Mararani, Kiangwe na Bodhei viko ndani ya msitu huo.

Mwenyekiti wa Wazee wa jamii ya Waboni, hasa wale ambao ardhi zao zilitwaliwa kufanikisha ujenzi huo wa barabara, Bw Ali Gubo, alieleza kutamaushwa kwake na jinsi serikali inavyoendeleza kimya kuhusiana na suala la kuwafidia.

Bw Gubo anasema wazee wengi tayari wamefariki bila ya kupokea fidia, hali ambayo inafukuzia mradi huo baraka.

Aliiomba serikali kuzingatia kilio chao na kuwafidia ili mradi huo usiendelee kugubikwa na laana.

“Hatuko radhi na mradi huo wa barabara. Kwa nini serikali kutudanganya tuache ardhi zetu kupisha ujenzi wa barabara na hata kutuahidi kwamba tungefidiwa, halafu inaturuka? Kila anayeulizwa kuhusu fidia zetu anatuzungusha tu miaka nenda miaka rudi. Wazee wenzetu wamefariki bila kuona fidia waliyosubiri muda wote. Inamaanisha hao waliofariki hawako radhi makaburini. Sisi pia tuko na kinyongo na mradi huo. Hatujatendewa haki,” akasema Bw Gubo.

Bw Hamisi Guyo alisema ni dhahiri nuksi inayoandama mradi tangu ulipoanzishwa karibu miaka minne iliyopita inatokana na duizo za jamii ya Waboni.

Bw Guyo alisema wakati umewadia kwa serikali kutambua ilikosea wapi na kufanya hima kurekebisha makosa hayo ili kuuwezesha mradi kutekelezwa kwa kheri.

“Utafauluje ikiwa wewe ni mwenye kudhulumu haki za wanyonge kama hii jamii yetu ya walio wachache? Mradi unaendelea kudumaa na endapo serikali haitatekeleza haki kwa huyu mwananchi maskini hapa mashinani huenda mradi ufeli kabisa. Twataka haki yetu ya fidia,” akasema Bw Guyo.

Kauli yake iliungwa mkono na Bi Mariam Tenee aliyelalamika kuwa baadhi ya Waboni waliofurushwa kutoka kwa ardhi zao kupisha ujenzi wa barabara hiyo wamesalia maskwota.

Aliiomba serikali kuwaonea huruma waathiriwa wa mradi huo na kuwafidia haraka iwezekanavyo ili na wao wajiendeleze maishani.

“Najua serikali imenyamazia suala hili la fidia kwa ardhi zetu ikijua fika kuwa Waboni wengi hawana hatimiliki za ardhi zao. Hizi ni ardhi za mababu zetu na hata kama hatuna stakabadhi, hicho si kigezo cha kutukosesha fidia. Watulipe ili tuwape radhi yetu,” akasema Bi Tenee.

Tangu ulipoanzishwa, mradi huo umeshuhudia makumi ya mashambulio ya magaidi wa Al-Shabaab ambayo kufikia sasa yameacha watu karibu 16 wakifariki.

Vifaa vya ujenzi wa barabara, ikiwemo matingatinga, malori, trekta na vinginevyo, ambavyo thamani yake ni zaidi ya Sh200 milioni pia vimeharibiwa kupitia kuteketezwa na Al-Shabaab kati ya 2021 na 2023.

Kufikia Julai mwaka jana, serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Barabara Kuu nchini (KeNHA) ilituma wahandisi ili kutathmini kazi kwenye mradi huo ambao mwanakandarasi wake ni kampuni ya China Communication Construction Company (CCCC) ambaye tayari alikuwa ameukamilisha kwa asilimia 53.4.

 

Picha ya barabara ya Lamu-Ijara-Garissa ambayo kwa ujumla ni ya umbali wa kilomita 453. Mradi huo unapitia katikati ya msitu wa Boni na uko Lamu na Garissa. PICHA | KALUME KAZUNGU

Jumla ya Sh9.8 bilioni ambazo ni zaidi ya nusu ya jumla ya fedha zilizotengenwa mradi wote ambao ni wa kilomita 453 pia zilikuwa zimetumika.

Baada ya ukaguzi kufanywa aidha, ilibainika kuwa kazi iliyokuwa imetekelezwa haikufikia viwango vya ubora vilivyowekwa, hivyo mwanakandarasi kuamriwa kuuanza upya kwa gharama yake mwenyewe.

Ni wakati huo ambapo serikali pia ilimpiga kalamu mhandisi mkuu msimamizi wa mradi huo, ambapo mwingine aliletwa.

Tangu kazi hiyo kuanzwa upya mwezi huu wa Februari, ni mita 200 pekee za barabara hiyo ambazo kufikia sasa zimejengwa na kupasishwa.

Kulingana na mhandisi mpya msimamizi wa mradi huo, Bw Willis Ingari, mita 200 zilizokamilishwa zilikuwa ni zile za majaribio.

Bw Ingari alisema anaamini endapo usalama utaimarishwa na mwanakandarasi kujituma vilivyo mradi huo utakamilika kwa wakati mzuri.

“Tayari mradi umechelewa kwa karibu miezi kumi sasa. Kazi iliyofanywa awali ilikuwa ya shagalabaghala, hivyo ikabidi mwanakandarasi akalazimishwa kuvunja na kuanza upya. Ninaamini serikali itaendelea kuzidisha ulinzi eneo hili ili wafanyakazi wawe na imani ya kukaa huko wakiendeleza ujenzi wa barabara hiyo,” akasema Bw Ingari.