Habari za Kitaifa

Linturi avuta mkia tena katika utendakazi wa mawaziri – Infotrak

June 11th, 2024 2 min read

NA JAEL MAUNDA

WAZIRI wa Kilimo Bw Mithika Linturi aliyeokolewa na bunge kuhusu kesi ya mbolea ghushi iliyokuwa ikimkabili ameorodheshwa kuwa waziri ambaye utendakazi wake ni duni zaidi.

Bw Linturi alipata asilimia 39 kati ya 100 ambayo ni alama ya E.

Akizungumuza jijini Nairobi, Meneja wa Masuala ya Nyanjani katika kampuni ya Infotrak, Bw Johvine Wanyingo, alisema kuwa idadi kubwa ya waliohusika kwenye utafiti uliofanywa wiki mbili zilizopita, unaonyesha kuwa waziri huyo ndiye anayechukuliwa kuwa asiyetekeleza majukumu yake ipasavyo.

“Watu 1,700 walihojiwa kwa njia ya simu kwa muda wa wiki mbili zilizopita. Ni watu wa umri wa kati ya miaka kumi na minane na zaidi. Utafiti huu ulifanywa katika kaunti zote 47. Asilimia 49 wakiwa wanawake, asilimia 51 wakiwa wanaume,” alisema Bw Wanyingo.

Aliongeza kuwa katika utafiti huo, walizingatia mambo yanayomwathiri mwananchi wa kawaida, na kuhusu uwezo wa mawaziri kufanya kazi walizopewa na Rais William Ruto.

“Tulitaka kujua iwapo mawaziri tulio nao wanaweza kuwasiliana na Wakenya na kuwajuza wanachokifanya na iwapo wanashughulikia masuala yanayowaathiri Wakenya. Pia tulitaka kujua iwapo mawaziri hao wanaweza kuboresha jinsi mambo yanavyofanywa katika wizara zao,” akasema.

Mwenzake wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki alipata asilimia 60 ambayo ni alama ya B, na kuibuka wa kwanza kwa mara nyingine.

Mawaziri tano bora wakiongozwa na Prof Kithure Kindiki ni Ababu Namwamba (Michezo), Aden Duale (Ulinzi), Soipan Tuya (Mazingira) na Eliud Owalo wa Teknolojia na mawasiliano. Naye Alfred Mutua (Utalii) alipata asilimia 47.

Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi na Waziri wa Elimu Bw Ezekiel Machogu pia walipata asilimia 47 sawa na Bw Mutua.
Lakini mwanasheria mkuu Justin Muturi alipata asilimia 46 akiwa na alama D.

Mawaziri walio nambari tano chini ni waziri wa umma Moses Kuria akipata asilimia 43, Simon Chelugui asilimia 43, Florence Bore wa Leba na Davis Chirchir wa Kawi k wakipata alama ya D.

Waziri wa Mazingira Bi Soipan Tuya ndiye mwanamke pekee katika orodha ya mawaziri kumi bora.

Infotrak pia walifanya uchunguzi kuhusu utendakazi wa raisi William Ruto ambaye alipata asilimia 46 akiwa na alama ya D ikilinganishwa na mwezi machi ambapo alipata asilimia 52 alama ya C naye naibu wake Rigathi Gachagua akipata asilimia 42 alama ya D.

Upinzani walipata asimia 47, mahakama ikipata asilimia 46, bunge wakipata asilimia 42 wote wakipata alama ya D.