Michezo

Makocha wa zamani wa Chelsea wanyakuliwa kama andazi moto

June 4th, 2024 1 min read

NAPOLI wanajiandaa kumjulisha rasmi Antonio Conte kama kocha wao mpya baada ya kutia saini mkataba wa miaka mitatu.

Conte atarejea Italia katika Serie A baada ya uzoefu wake katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) akiwa na Tottenham Hotspur.

Baada ya msimu mbaya, Napoli wataanza ukurasa mpya chini ya Conte, ambaye anarejea Serie A ya Italia miaka mitatu baada ya kuondoka.

Kocha huyo raia wa Italia alijiunga na Chelsea akiwashindia Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika mwaka wake wa kwanza.

Lakini alitimuliwa mwishoni mwa msimu wake wa pili licha ya kushinda Kombe la FA, kutokana na uhusiano mgumu na mmiliki wa wakati huo wa klabu hiyo Roman Abrahmovic.

Tangu Napoli waagane na Luciano Spalletti msimu 2023 wameteua mameneja watatu katika msimu uliopita (Rudi Garcia, Walter Mazzarri na Francesco Calzona).

Lakini hakuna hata mmoja amefanikiwa kuimarisha makali ya timu hiyo.

Kwa upande mwingine, klabu ya Fenerbahce ya Uturuki, imemtangaza rasmi kocha Jose Mourinho kama kocha wao mpya.

Maelfu ya watu walifika katika uga wa Sukru Saracoglu jijini Istanbul mnamo Jumapili kutazama Mourinho akijulishwa.

Mourinho 61, anachukua nafasi ya Ismail Kartal ambaye aliondoka Fenerbahce siku ya Ijumaa baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye ligi nyuma ya mahasimu Galatasaray, licha ya kupoteza mchezo mmoja pekee na kuzoa pointi 99 msimu huu.

Mourinho aliambia mashabiki wa Fenerbahce kuwa “shati hii ni ngozi yangu” alipotangazwa kama kocha wao mpya.

Mourinho amekuwa hana kazi tangu atimuliwe na Roma mwezi Januari baada ya kuionoa misimu miwili na nusu.

Kocha huyo wa zamani wa Chelsea, Real Madrid na Manchester United ndiye meneja pekee aliyeshinda kombe la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), kombe dogo la Europa League na kombe-toto la Europa Confernce League.